December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bunge limevunjwa: Wabunge, mawaziri bado ‘wanachapa kazi’

Rais John Magufuli

Spread the love

WABUNGE wa  Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wataendelea kutumikia na kutambulika katika nafasi zao za ubunge hadi tangazo rasmi la kuvunjwa kwa Bunge la 11, litakapotolewa kwenye Gazeti la Serikali (GN). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma …(endelea).

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge huvunjwa kwa hatua mbili.

Rais wa Jamhuri kuhutubia Bunge na kuchapishwa kwa taarifa hiyo kwenye GN. Kwa mujibu wa Ibara ya 65 (1) (2) ya Katiba, maisha ya kila Bunge, yatakuwa ni muda wa miaka mitano.

Kwamba, “maana ya neno, maisha ya Bunge,” katika Katiba ya Jamhuri inaeleza, “ni ule muda wote unaoanzia ambayo Bunge jipya limeitishwa ili kukutana kwa mara ya kwanza na kuishia tarehe ya kuvunjwa kwa Bunge kwa ajili ya kuwezesha uchaguzi mkuu mwingine wa kawaida kufanyika.”

Naye Spika wa Bunge na Naibu Spika wa Bunge, wataendelea na madaraka yao, hadi Bunge jipya litakapoitishwa.

Ibara ya 90 (1) ya Katiba, inamuelekeza Rais wa Jamhuri, “kuitisha mkutano wa Bunge jipya ufanyike kabla ya kupita siku saba tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu katika majimbo ya uchaguzi yote, isipokuwa majimbo yale uchaguzi utakuwa umefutwa na kutakiwa kufanyika upya.”

Akifafanua maana ya maneno “Rais amelihutubia Bunge na kutamka amelivunja,” mmoja wa maofisa wa sheria wa Bunge ambaye hakupenda kutajwa jina lake amesema, “pamoja na Katiba kutakamka Rais wa Jamhuri ya Muungano, atalihutubia Bunge na kulivunja, lakini hiyo haitoshi kuvunjwa kwa Bunge.”

Anasema, “ni sharti Rais akishasema, kwa mujibu wa sheria, pamoja na hotuba hiyo ya Rais ya kutangaza kulivunja Bunge, ili jambo hilo liweze kutekelezeka kwa mujibu wa sheria, ni sharti tamko lake hilo, lichapishwe kwenye GN (Gazeti la Serikali.”

Katika hotuba yake aliyoitoa juzi Jumanne tarehe 16 Juni 2020, Rais John Magufuli alisema,”…sasa natamka Bunge hili, litavunjwa rasmi kwa tarehe itakayotangazwa kwenye gazeti la Serikali.”

Hii inamaana kwamba, wabunge wataendelea kuitwa wabunge hadi pale Rais atakapotoa tangazo katika GN.

Mbunge wa Momba, David Silinde akizungumza na MwanaHALISI ONLINE amesema ubunge wao utakoma,”mpaka pale (Rais) atakapo vunja Bunge kwa kutoa taarifa katika GN ambayo inakuwa siku tatu kabla hatujaanza rasmi kampeni za uchaguzi.”

Silinde anaungana na Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa anayesema wanaendelea na majukumu, “Mpaka Mhe Rais akisaini instrument, kwa sasa bado ni wabunge na tunaendelea na kazi kama kawaida.”

Mchengerwa ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria amesema,”dhamira ni kuondoa ombwe la uongozi.”

Alipoulizwa kama wataendelea kupeperusha bendera za kibunge kwenye maeneo yao, Mchengerwa amesema,”Bendera Hapana! Lakini kwa mujibu wa katiba, wabunge wataendelea na Ubunge mpaka kuapishwa kwa wabunge wengine.”

“Kwa maana Katiba imetoa mwanya kwa wabunge kuweza kukutana wakati wowote iwapo yatatokea mambo kadhaa yaliyoelezwa katika Katiba na Wabunge watakutana iwapo mambo hayo yatatokea hatakama Bunge limeshavunjwa,” ameongeza.

Hii inakwenda sanjari na Baraza la Mawaziri ambapo mawaziri wataendelea kutumikia nafasi hizo hata pale ambapo tangazo la kuvunjwa kwa Bunge litatoka.

Hotuba hiyo ya Rais Magufuli la kulivunja Bunge ilitanguliwa na ile ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoitoa Jumatatu tarehe 15 Juni 2020 ya kumalizika kwa mikutano 19 ya Bunge hilo la 11 lililoongozwa na Spika, Job Ndugai na Naibu wake, Dk. Tulia Ackson.

error: Content is protected !!