RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imetenga Sh. bilioni sita kwa ajili ya kuiboresha Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi, mkoani Kilimanjaro. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa, tarehe 15 Oktoba 2021, mkoani Kilimanjaro na Rais Samia wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika hospitali hiyo.
Rais Samia amesema fedha hizo zimetengwa katika Mpango wa maendeleo kwa ustawi na mapambano ya UVIKO -19 ambao umetokana na mkopo nafuu wa Sh trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
“Juzi tulizindua mpango wa matengenezo ya hospitali za rufaa Tanzania nzima, pamoja na vituo vya afya. Hivyo Mawenzi imebahatika na kutengewa Sh bilioni sita na nimeoneshwa Mawenzi inavyotakiwa kuwa,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesema tayari Serikali imetoa Sh bilioni tatu ili kuendeleza ujenzi wa wodi hiyo.
“Ujenzi karibu unamalizika, najua kulikuwa na mkwamo tumeingiza Sh. bilioni tatu, nadhani ujenzi utaendlea na Sh. bilioni tatu zilizobaki tutazimalizia ili jengo likamilike,” amesema Rais Samia.
Leave a comment