January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Samia azindua barabara Kilimanjaro, mabango ya kero yatawala

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amezindua Barabara ya Sanya Juu- Elerai, iliyopo Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Samia amezindua barabara hiyo leo Ijumaa, tarehe 15 Oktoba 2021, katika ziara yake ya kikazi ymkoani Kilimanjaro na Arusha.

“Barabara hii ilikuwa ni kero ya siku nyingi na kama alivyosema mtendaji mkuu TANRODA, kwamba inajengwa kwa awamu, tumefanya awamu ya kwanza, hii ya pili na ya tatu ya kilomita 44 imebaki . Usanifu uko tayari, kilichobaki kutoa fedha na kumalizia,” amesema Rais Samia.

Aidha, akizindua barabara hiyo, baadhi ya wananchi walimpokea kwa mabango yenye kero , hasa za migogoro ya ardhi, ukosefu wa maji na maslahi ya wafanyakazi.

“Nilipita hapa Septemba na nikaahidi nitakuja fanya ziara. Sasa nipo kwenye ziara rasmi nimeanza na Kilimanjaro, baadae nitakwenda Arusha. Nimepita kuangalia yaliyotendeka lakini pia kuangalia changamoto zilizopo na hapa naona mabango mengi, kuna migogoro ya ardhi, maslahi ya wafanyakazi,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewaagiza wasaidizi wake, wakusanye mabango hayo ili kero zake zikatafutiwe ufumbuzi.

“Naomba maafisa wangu wakusanye yote halafu tutaenda kuyafanyia kazi, mbebe kama kawaida yetu tutakwenda kuyafanyia kazi,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewaagiza viongozi wa mikoa kutatua changamoto za wananchi, walioko katika maeneo yao, ili zisijirudie mara kwa mara.

“Niwaombe pale ambapo Serikali na chama wamekuja kuzunguzma nanyi wananchi na kutatua changamoto, naomba viongozi kusimamia utatuzi wake, haipendezi changamoto inatatuliwa ukija tena changamoto ileile ipo,” amesema Rais Samia.

Katika ziara yake hiyo, Rais Samia amesema atafungua daraja la Rau, kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la huduma za mama na mtoto, katika Hospitali ya Mawenzi mkoani Kilimanjaro.

Rais Samia Suluhu Hassan

“Leo kutwa nzima niko kwenye ziara, nikitoka hapa nakwenda kufungua daraja ambalo limejengwa maeneo ya Rau, lakini nitakwenda Hospitali ya Mawenzi ambako tunakwenda kuweka jiwe la msingi , la jengo kubwa la huduma za mama na mtoto, lengo kutoa huduma bora ili kupunguza vifo vya wanawake wakati wa kujifungua na mtoto,” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo wa Tanzania, amesema lengo la ziara yake hiyo ni kuangalia changamoto za wananchi, ili kuzifanyia kazi.

“Niwaahidi masuala ya elimu, afya, umeme na maji vijijini, yote tunakwenda kuyafanyia kazi. Juzi tumezindua mpango mkubwa sana wa kuleta maendeleo vijijini na kuondoa changamoto ziliopo. Bila shakaa Kilimanjaro na wenyewe wamepata mgawo wao, utakuja kwa wananchi kutatua changamoto,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewaomba Watanzania, kuendelea kudumisha utulivu na amani ili kuipa nafasi Serikali kufanya kazi ya kuwaletea maendeleo.

“Kazi ya kutafuta fedha nyingine kutatua changamoto ya wananchi inaendelea, nawaomba dumisheni amani na utulivu katika maeneo yenu, ili Serikali iweze kupata muda wa kufikiri, kutafuta fedha ili kumaliza changamoto zinazowakabili,” amesema Rais Samia.

error: Content is protected !!