October 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bei za petroli, dizeli Dar ‘buku jero’

Spread the love

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei mpya za mafuta ya Petroli, Dizeli na mafuta ya taa zitakazoanza kutumika kesho Jumatano tarehe 3 Juni 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne tarehe 2 Juni 2020 na Mhandisi Godfrey Chibulunje, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura imesema, bei hizo zimepungua ukilinganisha na bei za mwezi Mei 2020.

Amesema, bei za jumla na rejareja za mafuta ya Petroli na Dizeli yaliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam zimepungua ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe 6 Mei 2020.

Amesema, bei za Mafuta ya Taa zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita la tarehe 6 Mei 2020 kwani hakuna shehena ya mafuta hayo iliyopokelewa Mei 2020 kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Chibulunje amesema, Juni 2020, bei za rejareja za Petroli na Dizeli zimepungua kwa Sh. 348/lita (sawa na asilimia 18.65) kwa mafuta ya Petroli na Sh. 300/lita (sawa na asilimia 16.25) mafuta ya Dizeli.

Kwa bei hizo, wakazi za Jiji la Dar es Salaam, watanunua nishati hiyo kwa gharama isiyozidi Sh.1,500 ‘buku jero’ kwa mafuta ya petroli, dizeli au mafuta ya taa.

Bosi huyo wa Ewura amesema, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa kwa Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita la tarehe 6 Mei 2020.

“Hii ni kwasababu, kwa Mei 2020, hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Tanga,” amesema Chibulunje

Amesema, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya Petroli katika Mikoa ya Kusini (yaani Mtwara, Lindi na Ruvuma) hazitabadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe 6 Mei 2020 kutokana na kuwa hakuna shehena ya Petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara.

Chibulunje amesema, hata hivyo, bei za mafuta ya Dizeli zimepungua ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita.

Amesema, bei za jumla na rejareja za Dizeli zimepungua kwa Sh. 425/lita (sawa na asilimia 19.45) na Sh.423.24/lita (sawa na asilimia 20.58).

“Kwa kuwa hakuna Mafuta ya Taa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za Mafuta ya Taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutokea Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoa husika,” amesema

“Mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji (BPS Premium),” ameongeza

error: Content is protected !!