Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa AfDB kuendeleza ushirikiano na sekta ya nishati nchini
Habari za Siasa

AfDB kuendeleza ushirikiano na sekta ya nishati nchini

Spread the love

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kevin Kariuki kuhusu miradi mbalimbali ya umeme inayofadhiliwa na benki hiyo pamoja na miradi mingine ya nishati iliyo katika mpango wa kufadhiliwa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mazungumzo hayo ambayo yamefanyika leo tarehe 5 Februari 2024 Jijini Dodoma pia yamehudhuriwa na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba.

“Benki ya Maendeleo Afrika imeonesha nia ya kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo ya usafirishaji na usambazaji umeme.

“Pia wameamua kuweka kipengele cha nishati safi ya kupikia kwenye mipango yao, na hii ni katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033,” amesema Dk. Biteko.

Amesema AfDB imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo mradi wa umeme wa Kakono wa megawati 87.8 kwa kuchangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 161 na mradi wa Malagarasi wa megawati 49.5 kwa kuchangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 120.

Amefafanua kuwa, Benki hiyo pia imetoa sehemu ya fedha za utekelezaji wa miradi ya usafirishaji umeme ukiwemo mradi wa Singida-Arusha-Namanga (kV 400) ambao sasa umefikia asilimia 99.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kevin Kariuki (wa pili kushoto) na ujumbe wake alipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma leo Februari 05, 2024. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Pia imetoa fedha katika mradi wa Rusumo-Nyakanazi (94 km) ambao umekamilika kwa asilimia 100 na mradi wa umeme wa Backbone unaojumuisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme mkoani Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga ambapo kituo cha Dodoma na Singida vimekamilika kwa asilimia 100.

Kufuatia hatua hiyo, Dk. Biteko ameishukuru AfDB kwa kutoa sehemu ya fedha ambazo zinatekeleza mradi wa usafirishaji umeme wa kV 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma ambao sasa umefikia asilimia 92.

AfDB pia imeonesha nia ya kufadhili mradi wa usambazaji wa Gesi Asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam kwa kutumia mfumo wa ushirikiano na Sekta Binafsi (PPP).

Pia AfDB imeonesha nia ya kushirikiana na Serikali katika mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar ya kV 220 sambamba na kushirikiana na serikali katika uendelezaji miradi mbalimbali ya nishati jadidifu.

Dk. Biteko amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni fursa adhimu itakayowezesha Taifa kuwa na nishati ya kutosha kwa maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kevin Kariuki, amesema  nia ya Benki hiyo ni kuhakikisha miradi ya umeme inayofadhiliwa na AfDB inakamilika kwa wakati ili kuwapa wananchi umeme wa uhakika.

Ameongeza kuwa, Benki hiyo itaendelea kufanya tathmini kuona namna ya kuendeleza mipango mbalimbali ya Tanzania kwenye gesi asilia ikiwemo kupitia mpango mkakati wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili kuainisha maeneo zaidi ya ushirikiano.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!