Tuesday , 30 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Msigwa: Hakuna aliyeupinga, kufuta ujenzi bandari Bagamoyo
Habari za Siasa

Msigwa: Hakuna aliyeupinga, kufuta ujenzi bandari Bagamoyo

Spread the love

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema hakuna aliyewahi kuupinga wala kuufuta ujenzi wa bandari ya Bagamoyo chini ya mradi wa Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo (SEZ). Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea)

Msigwa ametoa kauli hiyo leo tarehe 13 Februari, 2022 wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari Visiwani Zanzibar waliotaka kufahamu hatima ya ujenzi wa bandari hiyo hasa ikizingatiwa imekuwa na ndimi mbili tofauti katika serikali ya awamu ya tanbo na ya sita.

Pia waandishi walitaka kufahamu hatima ya bandari jirani kama vile Mangapwani na Mtwara ambazo zinaweza kuathiriwa na ujenzi wa bandari hiyo ya Bagamoyo.

Akijibu maswali hayo, Msigwa amesema hiyo kumekuwapo na taarifa nyingin za upotoshaji kuhusu ujenzi wa bandari hiyo ya Bagamoyo.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan hakusema kwamba anarejesha ujenzi wa bandari ya Bgamoyo bali alisema tuzungumze kuhusu bandari.

“Na awamu ya tano hakusema bandari ya Bagamoyo tupa kule… alisema tuangalie manufaa ya bandari ya Bagamayo kwa masharti ambayo hayana manufaa na sisi tusitekeleze kwanza.

“Sasa Rais Samia alichokiagiza tukazungumze na wawekezaji, tuangalie masilahi yetu Tanzania yako wapi ndio tukatekeleze mradi,” amesema.

Aidha, amesema kumekuwa na mkanganyiko kuhusu ujenzi wa mradi huo ambao hata yeye (Msigwa) anahusishwa kuwa na ndimi mbili.

“Hakuna aliyeupinga au kuufuta, Msigwa ni yuleyule niliyesema kipindi kile na ninasema leo hivyohivyo,” amesisitiza Msigwa.

Aidha, amesema bandari hiyo ni mali ya Serikali hiyo mwekezaji atakayekuja atamkaribishwa kulingana na makubaliano ambayo Serikali inaona mwekezaji atapata na Taifa litapata.

Pia ameongeza kuwa Serikali haijengi bandari ya Bagamoyo ili kuuwa bandari ya Mangapwani au Mtwara.

“Tunachofanya ni kuwa na malango ya uhakika ya biashara … nchi yetu ni nchi ya kimkakati kwenye eneo la bandari. Tunapokuwa na bandari za uhakika tunalisha nchi ambazo hazina bandari,” amesema.

Pamoja na mambo mengine amesema kutokana na maagizo ya Rais Samia, mazungumzo kuhusu mradi huo yanaendelea na yatakapomilika Serikali itatoa taarifa kwa umma.

MRADI ULIANZIA HAPA

Mwezi Oktoba mwaka 2015, ujenzi wa mradi wa Bagamoyo chini ya Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo (SEZ), ulizinduliwa rasmi na Rais wa awamu ya nne wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete.

Kwenye uzinduzi huo alikuwepo Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Usultani wa Oman Dk. Ahmed Mohamed Al Furaisi na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya China Merchants Group Dk. Hu Jianhua kuashiria safari ya kuelekea kupata bandari itakayokuwa na uwezo karibu mara mbili ya Bandari ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa ndio tegemeo na bandari kubwa nchini.

Kabla ya uzinduzi kulikuwa na majadiliano na mazungumzo ya muda mrefu kuhusu thamani ya mradi wenyewe, uwekezaji, ubia, hasara na faida zake, lakini ziara ya mwezi Machi mwaka 2013 ya Rais wa China, Xi Jinping nchini Tanzania, na kusaini mikataba 16 na mwenyeji wake Rais Kikwete kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ilitoa picha ya namna utawala wa awamu ya nne ulivyoamini kuhusu mradi huu wa Bagamoyo na faida zake.

Aidha, kabla ya ujenzi kuanza Mwezi Mei, 2019 Serikali ililitaarifu Bunge la Tanzania kwamba mradi huo umefutwa na hautafanyika tena.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Maawasiliano (wakati huo), Isack Kamwelwe akiwasilisha hotuba yake tarehe 9 Mei, 2019 alisema majadiliano na wawekezaji hao yamesitishwa baada ya kuweka masharti yasiyokuwa na masilahi kwa Taifa.

“Masharti hayo ni pamoja na wawekezaji kudai kuachiwa jukumu la kupanga viwango vya tozo na kutoruhusu wawekezaji wengine katika eneo la kati ya Bagamoyo na Tanga,” alisema Kamwelwe.

Kauli ya Kamwelwe ilikuja baada ya wabunge kuchachamaa kuhusu mradi huo huku wakiungwa mkono na Spika Job Ndugai.

Aidha, tarehe 7 Juni, 2019 Rais wa awamu ya Tano, John e Magufuli aliueleza umma kwenye mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kwanini ameamua kufanya uamuzi huo.

Alinukuliwa akisema “kwenye mkataba wa ujenzi wa bandari hiyo kulikuwa na vipengele vya hovyo”.

Aidha, miaka miwili baadaye (tarehe 26 Juni, 2021), Rais Samia Suluhu aliutangazia umma kwenye mkutano mwingine wa Baraza la Taifa la Biashara kwamba ameamua kufufuwa ujenzi wa bandari hiyo.

“Tumeanza mazungumzo (na mwekezaji) ya kufufua mradi wote ule wa Bagamoyo ili nao tuufungue twende nao kwa faida ya taifa letu na kwa faida ya wawekezaji pia,” alisema Rais Samia.

Mradi huo unaohusisha maeneo kadhaa ya viwanda, mji wa kisasa wa makazi unaoendana na mahitaji ya karne ya 21, kituo cha usafirishaji, una thamani ya zaidi ya Sh23 trilioni.

Jiwe la msingi la mradi liliwekwa Septemba 2015 na Rais Kikwete, ambapo ulikuwa utekelezwe kwa ubia kati ya kampuni ya Merchant Holdings International Limited (CMHI) na State General Reserve Fund (SFRF) ya Oman.

1 Comment

  • Asante yale yale bendera haiwezi pepea bira ya upepo mkali kuwepo japo kuwa imesimamiwa and mlingoti

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

Habari za SiasaTangulizi

Samia ataja miradi ambayo Tanzania inashirikiana na IDA

Spread the loveRais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu amehutubia...

error: Content is protected !!