Tuesday , 30 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Mwinyi awapa ujumbe baraza la wawakilishi
Habari za Siasa

Rais Mwinyi awapa ujumbe baraza la wawakilishi

Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman
Spread the love

 

RAIS wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, amewataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutanguliza uzalendo wa kweli, ili kuisaidia Serikali na wananchi wa visiwani, kufikia maendeleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Ametoa wito huo leo Alhamisi, tarehe 23 Juni 2021, mjini Uguja, kupitia Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wajumbe wa baraza hilo, yenye lengo la kujenga uwezo wa wajumbe, katika ukumbi wa taasisi ya utalii, Maruhubi.

Dk. Hussein amesema, kumeshuhudiwa mara kadhaa kushuka kwa uadilifu kwa baadhi ya watumishi wa serikali yanayotokana na matatizo wanayokumbana nayo katika utekelezaji wa kazi zao.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

Alisema, ni muhimu kwa wajumbe hao, kujikita katika kuchunga maslahi ya nchi kwa kuzingatia uadilifu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, ili malengo ya serikali yaweze kufikiwa.

Ameongeza kuwa uwepo wa uzalendo kwa wajumbe hao utasaidia kukuza ufanisi kwa watumishi katika kusimamia majukumu yao hasa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya nchi pamoja na mambo yanayogusa maslahi ya kitaifa.

Akizungumzia majukumu, dhima na changamoto za baraza kimfumo na kitaasisi, Dk. Hussein amewahimiza wajumbe hao kujikita katika kuangalia namna ya kutafuta njia ya kukwamua matatizo yanayowakabili watumishi wa serikali na kuacha kuangalia makosa pekee yanayofanywa na watumishi hao.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar

Hata hivyo, amewatanabahisha wajumbe hao kuchukua tahadhari kwa baadhi ya mijadala inayohusu mahusiano ya Zanzibar na nchi nyengine kwa lengo la kulinda mahusiano hayo.

Aidha, Dk. Mwinyi ametoa wito kwa wahisani na wadau wengine mbalimbali wa maendeleo kuunga mkono Chuo cha Utawala wa Umma (IPA), katika kuendesha mafunzo hayo na kukiongezea mbinu za kiutendaji na kimiundombinu.

Akitoa nasaha zake kwa wajumbe hao, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, amewahimiza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutumia fursa hiyo katika kutoa michango yao ili lengo la kutolewa kwa mafunzo hayo lifikiwe.

Akitoa maelezo mafupi juu ya mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA), Dk. Shaaban Suleiman amesema, chuo hicho kimeamua kufanya mafunzo hayo kwa lengo la kuongeza uadilifu na uwajibikaji kwa watendaji wa serikali.

Ameongeza kuwa mpango huo ni katika njia za kuisaidia serikali kupunguza gharama za kuwapeleka nje ya nchi watendaji wake kwa ajili ya mafunzo na badala yake fedha hizo zitumike kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Katika mafunzo hayo, mada mbali mbali zimejadiliwa ikiwemo utumishi wa umma na utumishi wa kisiasa kwa mujibu wa sheria.

Mada nyingine, ni uzalendo na maslahi ya taifa; majukumu, dhima na changamoto za baraza kimfumo na kitaasisi, ambayo imebeba kaulimbiu ya “ushirikishwaji wa wananchi katika utungaji wa sera na sheria, ni kichochea cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Zanzibar.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

Habari za SiasaTangulizi

Samia ataja miradi ambayo Tanzania inashirikiana na IDA

Spread the loveRais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu amehutubia...

error: Content is protected !!