Thursday , 2 May 2024
Home Habari Mchanganyiko LSF yazindua mfumo wa kidigitali kutoa msaada kisheria
Habari Mchanganyiko

LSF yazindua mfumo wa kidigitali kutoa msaada kisheria

Spread the love

SHIRIKA linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji haki nchini Tanzania, kupitia uwezeshaji wa kisheria, Legal Services Facility (LSF), limezindua mfumo wa kidigitali wa kusaidia wananchi kupata msaada wa kisheria. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Mfumo huo wa kidigitali umezinduliwa leo Jumanne, tarehe 15 Juni 2021 na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Prof. Kabudi, amesema mfumo huo utasaidia kusogeza karibu huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi, hasa walioko maeneo ya vijijini.

“Leo nimefurahi kuona LSF wamekuja na mfumo ambao utasogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi, wanaohitaji huduma ya msaada na wasaidizi wa kisheria,” amesema Prof. Kabudi.

Waziri huyo wa Katiba na Sheria, amesema mfumo huo utasaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia, hasa kwa wanawake na watoto, kwani makundi hayo yatapa msaada wa kisheria kwa haraka, wanapokumbwa ukatili huo.

“Naamini kupitia mfumo huu wananchi wengi wakiwemo kina mama na watoto, wataweza kupata msaada wa haraka zaidi pale wanapokutana na changamoto mbalimbali, zinazohusiana na kuminywa ama kukandamizwa kwa haki zao, kutokana na jinsia au umri wao,” amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi amesema, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kushirikiana na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), ikiwemo LSF, kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria.
“Naipongeza sana LSF kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika suala hili la kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili na kwa kuendelea kutekeleza mradi wake mkubwa nchini Tanzania,” amesema Prof. Kabudi na kuongeza:

“Ambao kwa kiasi kikubwa umeweza kusaidia maelfu ya wananchi walio kwenye mazingira magumu, hususani wanawake na watoto kupata haki zao kutokana na kazi nzuri inayofanywa na wasaidizi wa kisheria nchi nzima.”

Akielezea utendaji wa mfumo huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala, amesema utapatikana katika simu za mkononi kupitia program ya ‘HAKI YANGU App’.

Ng’wanakilala amesema, huduma hiyo itapatikana nchi nzima, ambapo wananchi wataunganishwa na wasaidizi wa kisheria takribani 4,000, walioko maeneo yote Tanzania.

“Mfumo huo ni wa kwanza kubuniwa na wa aina yake nchini Tanzania, ambao utamsaidia mwananchi kuwasiliana moja kwa moja na msaidizi wa kisheria, au mtoa huduma za msaada wa kisheria, kupitia simu ya mkononi kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au kupiga simu,” amesema Ng’wanakilala.

Amesema mfumo huo utasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria wananchi.

“Kwa uzoefu wa LSF katika kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini, tumeona kuwa wananchi walio wengi bado wanakumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto,” amesema Ng’wanakilala.

Mtendaji huyo wa LSF ameongeza “hivyo njia hii itachochea upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi zaidi mahali popote kupitia simu ya mkononi.”

Mbali na uzinduzi wa mfumo huo, Ng’wanakilala amesema LSF itaendelea kushirikiana na NGO’s zaidi ya 200, zinazotoa huduma ya msaada wa kisheria nchi nzima, ili kuwasaidia wananchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yang’ara maonesho OSHA

Spread the loveBenki ya NMB imebeba tuzo ya kampuni bora kwenye sekta...

Habari MchanganyikoKimataifa

Ruto amteua Kahariri kuwa mkuu wa majeshi

Spread the loveRAIS wa Kenya, William Ruto, amemteua Jenerali Charles Muriu Kahariri,...

Habari Mchanganyiko

Chongolo aonya viongozi vijiji kutouza NIDA kwa wageni

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amewaonya viongozi wa...

Habari Mchanganyiko

TUCTA, OSHA wataka kampuni za madini kuiga ubunifu wa GGML

Spread the loveSHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) pamoja na Wakala...

error: Content is protected !!