Tuesday , 7 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Magufuli ampigia simu Majaliwa, atoa maagizo kwa mkandarasi
Habari za Siasa

Rais Magufuli ampigia simu Majaliwa, atoa maagizo kwa mkandarasi

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Magufuli amemuagiza mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation kutoka China aliyesaini mkataba wa ujenzi wa barabara kutoka Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilomita 53.2 kwa gharama ya Sh. 59.28 bilioni aanze kazi mara moja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Ruangwa … (endelea)

Ametoa agizo hilo leo Jumamosi, tarehe 27 Juni 2020 alipozungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi kwa simu alipompigia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa tukio la utiaji saini mkataba wa makubaliano ya ujenzi wa barabara ya hiyo kwa kiwango cha lami.

“Nashukuru ahadi niliyoitoa leo imeanza kuzaa matunda na ilimradi mkandarasi amekubali kusaini aanze mara moja kupeleka mitambo kwenye eneo la mradi na nitakuja kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo.”

Pia, Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kumpongeza Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa kwa uhodari wake katika kufanya kazi.

“Endeleeni kumuani Mheshimiwa Majaliwa, amekuwa akinisaidia. Aendelee kuchapa kazi kwa ajili ya Ruangwa na Tanzania.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu imesema, Majaliwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kuthamini na kujali maendeleo ya Watanzania wakiwemo na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwa sababu ujenzi wa barabara ya Ruangwa hadi Nanganga kwa kiwango cha lami ni utekelezaji wa ahadi yake.

“Leo hii ni siku ya kihistoria kwa sababu, kile ambacho tulikuwa tunatamani, kikaahidiwa hapa na kiongozi wa nchi Rais wetu John Pombe Magufuli alipofanya ziara Ruangwa aliweza kuvunja kiu yetu Wana-Ruangwa toka alivyokuwa anaingia Nanganga wananchi walimuomba asimame na yeye alisimama akijua kuwa hawa wana hamu ya maendeleo.”

Waziri mkuu amesema baada ya Rais Magufuli kusimama  aliwaambia kuwa “najua hamu yenu ni ya maendeleo, lakini mimi ninaanza kuwaondolea kiu ya muda mrefu ya barabara yenu kutoka hapa Nanganga mpaka Ruangwa kwa kuijenga kwa kiwango cha lami. Sifa moja ya Rais Magufuli ni kusema na kutenda na ametekeleza.”

Vilevile, waziri mkuu amewataka Watanzania wote waendelee kushirikiana bila ya kujali itikadi zao za kisiasa kwa sababu maendeleo hayana chama na miradi ya maendeleo anayoitekeleza katika maeneo mbalimbali nchini imekuwa ikiwanufaisha wananchi wote.

Rais John Magufuli

Akizungumzia kuhusu Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation kutoka China iliyosaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nanganaga kwa kiwango cha lami, Majaliwa amesema ni miongoni mwa kampuni kubwa zinazojenga kwa viwango.

Waziri mkuu ameendelea kuwashukuru wananchi wa wilaya hiyo kwa umoja na mshikamano mkubwa waliompatia katika kipindi chote cha miaka mitano na amewaahidi kuendelea kuwatumikia bila ya ubaguzi wa aina yoyote na kwamba waendelee kuiunga mkono Serikali ambayo imefanikiwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 kwa vitendo.

Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Ujenzi, Dk. Elias Kuandikwa amesema, barabara hiyo itakuwa na madaraja makubwa matatu na makaravati 31 na kwamba itajengwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyohitajika.

Dk. Kuandikwa amesema, barabara zingine za mkoa wa Lindi zikiwezo za kutoka Nachingwea hadi Liwale yenye urefu wa kilomita 159 ipo katika hatua ya usanifu na barabara ya kutoka Liwale hadi Nangurukuru kilomita 230 na Nanganga-Nachingwea-Masasi zipo katika utaratibu wa ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mapema, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale alisema barabara ya Nachingwea – Ruangwa – Nanganga ni barabara muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Lindi  kwani inaunganisha pia mkoa wa Lindi na mikoa jirani kwa barabara kuu ya Mtwara – Dar es Salaam na Mtwara – Masasi – Songea.

“Ili kurahisisha utekelezaji, mradi huu umegawanywa katika sehemu mbili: Sehemu ya Nachingwea hadi Ruangwa yenye urefu wa kilometa 52.8 na sehemu ya pili ni kutoka Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 53.2.”

“Serikali imeamua kuanza ujenzi wa sehemu ya Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 53. 2 na upana wa meta 10.0, kwa kutumia fedha za ndani na itajengwa kwa muda wa miezi 27,” alisema.

Mhandisi Mfugale aliongeza ujenzi wa barabara hiyo utakapokamilika utasaidia kukuza kilimo na utalii katika wilaya ya Ruangwa na mkoa wa Lindi kwa ujumla.

Aidha mradi utakapokamilika utachochea ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi waishio maeneo ya Ruangwa, Nanganga na Nachingwea.

Wakizungumza kuhusu ujenzi wa barabara hiyo wananchi wa wilaya ya Ruangwa walimshukuru Rais Magufuli pamoja na Majaliwa kwa uamuzi wao wa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani itasaidia katika ukuaji wa uchumi.

Miongoni mwa wananchi hao ni pamoja na dereva wa basi litokalo Ruangwa kwenda Masasi, Omar Njinji ambaye amesema, kutengenezwa kwa barabara hiyo kutarahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo, pia nauli zitapungua na maendeleo ya wilaya nayo yataimarika.

Dereva mwingine Issa Lingonda wanaishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kujenga barabara hiyo kwa sababu ubovu wake unasababisha magari kuharibika mara kwa mara.

“Tunamshukuru sana Rais pamoja na Mbunge wetu kwani tutapumzika kwenda gereji maana siku mbili tunafanyakazi siku mbili gereji. Ikiwekwa lami vyombo vyetu vya usafiri vitadumu na nauli zitapungua.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mpina mwiba CCM, ahofia kuzibwa mdomo

Spread the loveWAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM), kikijinasibu kuwa kinara wa demokrasia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mabeyo ametuepusha

Spread the loveNIMEGUSWA na uadilifu, utiifu na uaminifu wa Mkuu mstaafu wa...

Habari za SiasaTangulizi

CCM yaitaka TAKUKURU kuichunguza Chadema tuhuma alizoibua Lissu

Spread the loveCHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana...

error: Content is protected !!