August 4, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Upinzani washinda Urais Malawi

Lazarus Chakwera, Rais wa Malawi

Spread the love

LAZARUS Chakwera, Kiongozi wa upinzani nchini Malawi, ameibuka mshindi wa Urais katika uchaguzi wa marudio nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu kwa msaada wa mashirika ya kimataifa…(endelea).

Tume ya Uchaguzi Malawi (MEC) imesema, Chakwera amemshinda Rais aliyepo madarakani, Peter Mutharika kwa asilimia 58.57.

Uchaguzi huo umefanyika Jumanne iliyopita tarehe 23 Juni 2020 baada ya ule wa awali, uliofanyika Mei 2019 kufutwa na Mahakama nchini humo Februari 2020 kutokana na kubainika ulitawaliwa na dosari.

Katika uchaguzi huo wa Mei 2019, Rais Mutharika aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 38.57 huku Chakwera akipata asilimia 35.41.

Hata hivyo, Chakwera hakukubali matokeo hayo na kuamua kufungua kesi mahakamani kuyapinga na Februari 2020 akashinda kesi hiyo na uchaguzi ukarudiwa na yeye kuibuka mshindi.

Baada uamuzi huo wa Mahakama, Rais Mutharika alikwenda mahakama ya rufaa kupinga uamuzi huo ambapo hakufanikiwa kushinda.

Raia wa Malawi aipiga kura ya kumchagua Rais

Kilichotokea Malawi kufutwa kwa matokeo kinafanana na kile kilichofanywa na Mahakama ya Juu nchini Kenya mwaka 2017 kufuta matokeo yaliyokuwa yamempa ushindi Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, uchaguzi wa marudio ulipofanya, mgombea wa upinzani, Raila Odinga aliyefungua kesi hiyo hakushiriki na Rais Kenyatta kuibuka mshindi katika uchaguzi ambao haukuwa na upinzani mkali.

Mara baada ya kutangazwa mshindi wa Urais wa Malawi katika Taifa hilo la Bara la Afrika, Chakwera amesema,”ushindi wangu ni ushindi wa demokrasia na haki. Roho yangu imejaa furaha.”

Chakware mwenye miaka 65 amesema hayo usiku wa manane kuamkia leo Jumapili wakati akisherekea ushindi huo katika mitaa ya Mji wa Lilongwe.

Taarifa kutoka Malawi zinasema, Chakwera aliyekuwa anawakilisha vyama zaidi ya vitano vya upinzani, anatarajiwa kuapishwa leo Jumapili tarehe 28 Juni 2020.

Ushindi wa upinzani dhidi ya Rais aliye madarakani, hususan Bara la Afrika, unatoa funzo kwa nchi zingine barani humo kuzifanya Mahakama na tume zinazosimamia uchaguzi zinakuwa huru.

Baadhi ya mataifa ikiwemo Tanzania, matokeo ya Urais yakishatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hayawezi kuhojiwa au kupigwa mahakamani.

Kitendo hicho kimekuwa kikipingwa na wadau mbalimbali hasa wanasiasa wa upinzani wakitaka matokeo hayo ya urais yahojiwe mahakamani na uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi ambayo watumishi wake hawatoteuliwa na Rais.

Uwepo wa tume huru na matokeo hayo kupigwa mahakamani, kunafanya uchaguzi kuwa wa huru na haki na mgombea asiyeridhika kuwa na fursa ya kutafuta haki yake mahakamani.

Aliyekuwa Rais wa zamani wa Malawi, Peter Mutharika akipiga kura katika uchaguzi huo

Hata hivyo, Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli mara kadhaa amekuwa akisema, atahakikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 utakuwa wa amani, huru na haki.

Kauli ya mwisho kuitoa ilikuwa tarehe 16 Juni 2020 jijini Dodoma, wakati akilihutubia Bunge la 11 aliwaomba wagombea kutumia lugha za staha wakati wa kampeni na kuepuka maneno ya kejeli.

Uchaguzi wa Malawi unatoa funzo pia kwa vyama vya upinzania kwamba kama vitaungana au kushirikiana kwa dhati dhidi ya chama kilichopo madarakani vinaweza kuking’oa kama ambavyo imetokea Malawi.

Pia, suala la tume huru ya uchaguzi inaifanya kutenda haki na kumtangaza aliyeshinda pasina shaka kama ilivyotokea mwaka 2017 nchini Gambia kwa kiongozi wa upinzani, Adama Barrow alipotangazwa mshindi dhidi ya Yahya Jammeh aliyekuwa Rais kwa kipindi kirefu.

Uchaguzi huo wa Malawi, yanairejesha nchi hiyo kama yale yaliyotokea mwaka 1994 wakati Dk. Kamuzu Banda aliyetawala tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1964, alipokubali matokeo aliposhindwa na Bakili Muluzi.

Mafanikio hayo ya mwaka 1994 hayakuendelea tena na kuifanya Malawi kuwa katika mgogoro wa kisiasa baada ya Rais wa tatu wa Malawi, Bingu wa Mutharika kufariki duania Aprili 2012.

Baada ya kifo hicho, Rais wa sasa, Peter Mutharika ambaye ni ndugu wa Bingu alitaka kumzuia Joyce Banda aliyekuwa makamu wa Rais asiwe Rais kuchukua nafasi ya Bingu kwa mujibu wa Katiba ili kumalizia kipindi kilichokuwa kimebaki cha miaka miwili.

Hata hivyo, baada ya Rais Joyce kumaliza kipindi cha miaka miwili mwaka 2014, alikutana na upinzani mkali kutoka kwa Peter Mutharika na Joyce kuamua
kuunda chama kipya cha People´s Party.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI ONLINE & MwanaHALISI TV

error: Content is protected !!