MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imesema Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee anayekabiliwa na kesi ya uchochezi kwa kutoa maneno ya kuudhi dhidi ya Rais John Magufuli ana kesi ya kujibu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi tarehe 28 Mei 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Hakimu Simba amesema, mahakama hiyo imemkuta Mdee na kesi ya kujibu na kwamba anatakiwa kuwasilisha utetezi wake mahakamani hapo
Uamuzi huo umetokana na upande wa mashtaka kufunga pazia la ushahidi wake tarehe 20 Februari 2020.
Mdee kupitia wakili wake, Hekima Mwasipo amedai mteja wake atajitetea kwa kiapo na atakuwa na mashahidi watano.
Inadaiwa tarehe 3, Julai 2017, katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) iliyopo mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Mdee anadaiwa kutamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa, “anaongea hovyohovyo, anatakiwa afungwe breki” na kwamba kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Mdee alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza tarehe 10 Julai 2017, na kushtakiwa kwa mashtaka ya uchochezi.
Leave a comment