Sunday , 28 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kilichotarajiwa Burundi chatimia, wapinzani wang’aka
Habari za Siasa

Kilichotarajiwa Burundi chatimia, wapinzani wang’aka

Evariste Ndayishimiye, Rais wa Burundi
Spread the love

UCHAGUZI Mkuu nchini Burundi umefikia tamati, malalamiko yanayotolewa na vyama vya upinzani baada ya Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye wa chama tawala – CNDD-FDD – kutangazwa mshindi, yalitarajiwa. Inaripoti mitandao ya kimataifa…(endelea).

Tume ya Uchaguzi ya Burundi jana Jumatatu tarehe 25 Mei 2020, ilimtagaza Ndayishimiye kushinda kiti cha urais kwenye uchaguzi huo kwa kupata asilimua 68.72 ya kura, mpinzani wake Agathon Rwasa (CNL) akitajwa kupata asilimia 24.19 na kwamba, asilimia 88 ya walioandikishwa, walipiga kura.

Ndayishimiye aliyezaliwa mwaka 1968, atachukua nafasi ya Rais Pierre Nkurunziza, ambaye ameliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa miaka 15.

Kutangazwa kwa ushindi wa Ndayishimiye kumeiingiza Burundi kwenye hali ya wasiwasi. Kabla ya uchaguzi huo, wasiwasi unaoonekana sasa ulitabiriwa na wachambuzi wengi ndani na nje ya taifa hilo kutokana na maandalizi ya uchaguzi huo na ukandamizaji wa vyama pinzani.

Tayari vyama pinzani hasa CNL vimegomea matokeo hao. Vinaitaja Tume ya Uchaguzi kama ‘mhimili’ wa kuvuruga uchaguzi, vinaelekeza mashambulizi yake kwa utawala wa Rais Nkurunziza kwamba tayari walikuwa na mshindi wao.

Pierre Nkurunziza, Rais mstaafu wa Burundi

‘Kinachoimbwa’ na wapinzani kilielezwa na Prof. Karuti Kanyinga wa Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya kwamba, itakua ajabu ya dunia iwapo Nkurunziza na jeshi lake wataafiki Tume ya Uchaguzi ya Burundi kumtangaza mpinzani hata kama atashinda.

“Kwa Burundi, uchaguzi unafanyika ilimradi tu kujiwekea hadhi,” alisema Prof. Kanyinga kabla ya uchaguzi huo na kuongeza “jeshi na chama tawala, haviwezi kuruhusu mtu mwingine yeyote atangazwe kuwa mshindi, upinzani watagomea matokeo na yanaweza kujitokeza yale ya 2015.”

Kinacholalamikiwa na Rwasa baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo, ilielezwa na Lewis Mudge, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Hakiza Binadamu Afrika ya Kati kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Mudge alisema, mazingira ya uchaguzi huo yanaonesha wazi kwamba, serikali ina ‘mshindi’ wake na hivyo haikuwa tayari kuingiliwa na taasisi yoyote ndani na nje ya taifa hilo.

“Hakuna shaka kuwa, uchaguzi huu utafuatana na dhuluma zaidi, kwani maofisa wa Burundi na wanachama wa Imbonerakure (chama tawala), wanatumia vurugu bila chochote kushinikiza chama tawala kibaki madarakani kwa namna yoyote ile,” alisema siku mbili kabla ya uchaguzi huo.

Alisema, “vurugu na ukandamizaji vimekuwa ishara kuu ya siasa nchini Burundi tangu mwaka 2015, wakati huu tunakaribia uchaguzi, kuna maradhi ya corona, vyote hivyo vinazidisha hofu.”

Abdullahi Halakhe Boru, mchambuzi wa masuala ya siasa za Afrika alisema, kutokana na mazingira yalivyo, chama cha serikali ‘lazima kishinde.’

“Burundi imebaki yenyewe, Umoja wa Afrika haupo, wachunguzi wa kimataifa hawapo, watashinda tu,” alisema.

Therence Manirambona, msemaji wa (CNL) amesema, msimamo wa chama hicho ni kupinga matokeo hayo na kuhakikisha watafanya wawezalo ili kutafuta haki hiyo kwa kutumia vyombo vya sheria.

Amesema, uchaguzi ulioendeshwa na tume hiyo ulijaa udanganyifu, dhuluma na ukiukwaji wa haki za wananchi kuchagua wamtakaye na kuwa, aanaamini CNL kimechaguliwa na wananchi kwa kishindo.

“Tuna ushahidi wote na idadi kamili ya kura tulizopata kwenye uchaguzi huu. tutasaka haki yetu kwenye vyombo vya sheria,” Manirambona ameueleza mtandao wa ‘German news agency.’

Kabla ya Tume ya Uchaguzi kutoa matokeo yake, Rwasa alisema data zinalizokusanywa na chama chake zinaonesha kumshinda Ndayishimiye kwa mbali.

Ndayishimiye anatarajia kuapishwa mwishoni mwa Agosti na kuwa mwisho wa urais wa Nkurunziza, rais huyo atahudumu taifa hilo kwa miaka saba kwa mujibu wa Katuba ya taifa hilo.

Hata hivyo, haijafahamika kama Ndayishimiye ataongoza taifa hilo bila kuingiliwa na Nkurunziza ambaye anaonesha nia na tamaa ya ‘kuongoza’ taifa hilo nyuma ya pazia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

error: Content is protected !!