September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ongezeko matumizi mabaya ya mitandao yatua bungeni

Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga

Spread the love

MBUNGE wa Ulanga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Goodluck Mlinga ameihoji Serikali ya Tanzania jinsi ilivyojipanga kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Mlinga ameuliza swali hilo leo Jumanne tarehe 26 Mei, 2020 bungeni kwa njia ya mtandao kwa wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano ambaye naye amelijibu kwa mfumo huo huo wa kidigitali.

“Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile uchochezi, upotoshaji, udhalilishaji. Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo hilo,” ameuliza Mlinga

Akijibu swali hilo, Waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano amesema, Serikali tayari imechukua hatua kadhaa kwa ajili ya kuweka mazingira salama kwa wananchi hususan kwenye mitandao.

Amesema, Mwaka 2015 Serikali ilitunga sheria ya miamala ya kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala inayofanyika kimtandao; na sheria ya makosa ya Mitandao kwa lengo la kutambua kisheria makosa yanayofanyika kwenye mitandao ili kuweza kuchukua hatua stahiki yanapobainika makosa hayo.

“Pia, katika kujenga mazingira salama ya kisheria, Serikali iko kwenye mchakato wa kutunga sheria ya kulinda taarifa binafsi ambayo lengo kuu ni kuweka utaratibu wa ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi ili kupunguza matumizi mabaya ya taarifa hizo,” amesema waziri huyo

Amesema, Serikali ilianzisha Kitengo cha Uhalifu wa Mitandao (Cybercrime Unit) chini ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa makosa ya mitandao ikiwemo uchochezi, upotoshaji na udhalilishaji mtandaoni na kuandaa majalada ya kufungulia mashtaka kwa kusaidiana na kurugenzi ya mwendesha mashtaka.

Katika majibu hayo, waziri amesema, Serikali kupitia sheria ya mawasiliano ya kielektroniki na posta ilianzisha kitengo cha uratibu, ufuatiliaji na usimamizi wa matukio yanayotokea kwenye anga ya mtandao (TzCERT) ambayo iko chini ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

“Kitengo cha TzCERT kinashirikiana kwa ukaribu na taasisi nyingine za hapa nchini, taasisi za kikanda na kimataifa kupeana taarifa za kiintelijensia kuhakikisha anga ya mtandao inakuwa salama,” amesema

Amesema, wizara imeandaa Mkakati wa Taifa wa Usalama wa Mitandao wa mwaka 2018 ambao unaweka bayana mikakati ya kukabiliana na uhalifu wa mitandao.

“Serikali itaendelea kujengea uwezo watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama wa kukabiliana na matukio ya kimtandao, kuweka mifumo thabiti ya kukabiliana na matukio ya kimtandao, kuboresha mazingira ya kiudhibiti ili kuongeza ufanisi wa usimamizi wa matumizi mabaya ya mitandao hususan mitandao ya kijamii na kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao,” amesema

error: Content is protected !!