Thursday , 2 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Anywa soda 24 kwa saa moja
Habari Mchanganyiko

Anywa soda 24 kwa saa moja

Salum akiendelea na zoezi la kunywa soda
Spread the love

MTU aliyetambulika kwa jina moja la Salum, amesababisha shughuli mbalimbali kusimama katika eneo la maduka yaliyopo pembeni ya kituo cha mabasi cha Makumbusho jijini Dar es Salaam, baada ya kunywa kreti moja la soda ili kutimiza masharti ya kupewa Sh. 50,000/=, anaandika Charles William.

Tukio hilo limetokea leo, ambapo mtu huyo alikuwa akinywa vinywaji katika mojawapo ya duka la vinywaji (grocery), lililopo eneo la Makumbusho kabla ya kuingia kwenye ubishani na mteja mwingine juu ya uwezo wake wa kunywa kinywaji aina ya soda.

“Walikuwa wanabishana na mwenzake. Huyo jamaa akasema ana uwezo wa kunywa kreti zima la soda kama akipewa Sh. 50,000/=. Wakawekeana dau, ndiyo unaona mpaka sasa amebakisha soda tano tu,” alieleza mmoja wa mashuhuda wakati mwandishi wa habari hii alipofika eneo la tukio.

Wakati tukio hilo likiendelea, watu wengi walijaa na hivyo kusababisha wapita njia nao kuweka kambi katika eneo hilo kwa muda. Salum aliendelea kunywa soda hizo moja baada ya nyingine, akichanganya na maji kidogo.

Baadhi ya watu waliingiwa na hofu kuwa huenda mtu huyo akapata madhara, hasa kutokana na sharti la kutakiwa kumaliza soda hizo ndani ya saa moja (dakika 60).

Kutokana na hofu hiyo, mtu aliyeweka dau la Sh. 50,000/= iwapo Salum atamaliza soda hizo zote, aliamrisha watu kutoendelea kuchukua picha za tukio hilo, huku muuzaji wa duka hilo naye akimuomba mnywaji kutoendelea kunywa vinywaji kama anajihisi kutosheka.

“Jamani kama tayari tumbo limejaa usiendelee kunywa, usije ukapatwa na matatizo na ukashindwa hata kunyanyuka hapo kwenye kiti,” alisema dada huyo kwa hofu.

Hata hivyo Salum huyo aliendelea kunywa vinywaji hivyo mpaka alipomaliza na kukabidhiwa Sh. 50,000/= kama alivyoahidiwa. Kati ya fedha hizo alitumia Sh. 14,400/= kulipia soda hizo 24 kwa muuzaji, huku fedha zilizobakia akiondoka nazo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NEMC yatoa elimu matumizi sahihi ya zebaki kwa wachimbaji

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Oryx gesi yagawa mitungi, majiko 100 kwa waandishi wa habari Dar

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gesi Tanzania imegawa mitungi 100 ya gesi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari MchanganyikoMichezo

Wanamichezo Mei Mosi wachangia wahitaji vitu vya mil. 11.5

Spread the loveWanamichezo wanaoshiriki Michezo ya Mei Mosi Taifa 2024 jijini Arusha...

error: Content is protected !!