Wednesday , 8 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Ukatili wa watoto, Tamwa yaiangukia jamii na Serikali
Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ukatili wa watoto, Tamwa yaiangukia jamii na Serikali

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben
Spread the love

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimelaani matukio ya ukatili wa kijinsia yanayoendelea nchini huku kikiitaka Serikali na wananchi kutafuta mwarobaini wa changamoto hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo wa TAMWA umetolewa leo Alhamisi tarehe 12 Novemba 2020 na kwa  Mkurugenzi Mtendaji wake, Rose Reuben.

Taasisi hiyo imewaomba Watanzania kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha matukio hayo yanakomeshwa, ikiwemo jamii kuripoti visa vya ubakaji na mamlaka husika kuwachukulia hatua wahalifu.

“TAMWA tunaendelea kusisitiza uwazi na uwajibikaji katika kuripoti masuala ya ubakaji wa watoto. Kila mmoja atimize wajibu wake, familia, jamii, na watoto wenyewe wafundishwe kuvunja ukimya na wadau watumie nafasi walizonazo kuhakikisha ubakaji huu unamalizwa, serikali nayo itimize wajibu wake kisheria na usimamizi wa kesi za ubakaji kwa wakati,”  inaeleza taarifa ya Rose

TAMWA imeitaka jamii kutoiachia Serikali jukumu la kudhibiti matukio ya ukatili kwa watoto.

“Vita hii si ya serikali peke yake, bali na hata wadau wengine wote wa masuala ya ukatili wa jinsia na wa watoto, nia ikiwa ni kupunguza na kuzuia kabisa vitendo vya ukatili kwa watoto,” anasema Rose

Wito huo wa TAMWA umetolewa kufuatia kukithiri matukio ya ukatili wa kijinsia hasa ubakaji kwa watoto wadogo, licha ya uwepo wa sheria na sera zinazopinga ukatili huo.

“Hivi karibuni, vyombo vya habari vimeripoti matukio kadhaa ya ukatili wa kijinsia hasa ubakaji wa watoto yanayoashiria bado vitendo hivi vinaendelea licha ya kuwepo sheria, matamko na sera zinazopinga vikali matukio hayo,” anasema Rose.

TAMWA imetaja baadhi ya matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa hivi karibuni ikiwemo la Mwenyekiti wa Kijiji cha Ijinga, Wilaya ya Magu, Badri  Masengo (40) anayedaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Ijinga mwenye umri wa miaka 15 lililoripotiwa tarehe 11 Novemba 2020.

Tukio jingine ni  la mtoto wa miaka 6, wa Shule ya msingi Themi, jijini Arusha, aliyebakwa hadi kufa, Julai 2020. Pamoja na tukio la mtoto wa miaka 12 kubakwa na kujeruhiwa vibaya, wilayani Serengeti, lililotokea tarehe 12 Januari, 2020.

Tukio lingine ni la kubakwa kwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Monfort (10), aliyebakwa na mwalimu wake, Anderson Eneza (27), tarehe Novemba 11, 2020.

Pia, TAMWA imesema tukio lingine lilitokea tarehe 12 Agosti 2020 linalodaiwa kufanywa na  Medadi Chitezi (60) mkazi wa Kijiji cha Ulumi, Rukwa, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 10.

“Huko visiwani Zanzibar, limeripotiwa tukio la Mzee wa miaka 60, Haroub Abdallah Hamad, anayedaiwa kumbaka mtoto wa miaka mitano. Tukio hilo limetokea Oktoba 10, 2020, wilayani Wete, Pemba,” imesema taarifa ya Rose.

Taarifa hiyo ya Reuben imesema “Hivyo basi, TAMWA ambayo miongoni mwa malengo yake makuu ni kuzuia na kupunguza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, inalaani vikali kuendelea kwa matukio hayo katika jamii.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoMichezo

Kengold wakabidhiwa kombe NBC Championship

Spread the loveMdhamini mkuu wa Ligi Daraja la Kwanza (NBC Championship) Benki...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Kuanzia Agosti marufuku kutumia mkaa, kuni

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mwendokasi Kigogo – Segerea kujengwa awamu ya 5

Spread the loveNaibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Festo Dugange...

error: Content is protected !!