Lugola amesema hayo wakati wa uzinduzi wa ofisi ya kituo cha LHRC jijini Dodoma, ulioambatana na maadhimisho ya miaka 24 tangu kuanzishwa kwake.
Amesema Serikali inatambua harakati na mchango wa kituo hicho katika kulinda na kutetea haki za wanyonge, hivyo ni wajibu wa mamlaka husika ambayo ni msimamizi mkuu wa haki kuonyesha ushirikiano kwa vitendo.
“Yapo mambo mengi ambayo yanahitaji usaidizi katika nchi hasa masuala ya kisheria, na kwa kutambua juhudi za wadau wapigania haki ndio maana leo hii tupo hapa ili kutoa hamasa na kufikia lengo,” alisema Lugola.
Aidha ameongeza kuwa Serikali inatambua wajibu wake katika kulinda haki za binadamu, na kwamba ni lazima kuwajengea watanzania uwezo wa kutambua, kutetea na kulinda haki zao.
“Kwanini tunafanya hivyo, ni kwa sababu kupata haki za msingi ni wajibu wa kila raia ili mradi mtu huyo asivunje sheria na anafuata misingi ya Demokrasia kwa kuzingatia Utawala wa Sheria,” aliongeza Lugola
Awali akiongea katika ufunguzi wa ofisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo Cha Sheria na haki za binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga, amesema ili kulinda haki za binadamu wanaunga mkono juhudi za serikali katika kutimiza azma ya Tanzania ya viwanda inayoendana na utawala bora.
Henga amesema pia wanafurahishwa na juhudi za Serikali katika kukemea na kuchukua hatua kwa baadhi ya viongozi wasiokuwa na weledi, ambao huchafua taswira ya utawala wa kisheria, ikiwemo kupungua kwa ajali za barabarani.
“Pamoja na uwajibikaji pia moja kati ya mafanikio tunayojivunia ni kupunguza ajali za barabarani kutokana na kubadilisha mitizamo hasi ya watumiaji wa barabara kwa kuwafundisha utii wa Sheria bila shurti,” amesema Henga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa LHRC aliyemaliza muda wake Hellen Kijo Bisimba, amewataka wafanyakazi wa kituo hicho, kufanya kazi kwa weledi na kufuata misingi haki kwa kila mmoja bila kubagua.
“Malengo ya LHRC ni Pamoja na kuwafikia watanzania walioko pembezoni ambao hawajui namna ya kutafuta haki zao, hivyo ni lazima kufanya kazi kwa kufuata misingi na taratibu husika,” alisema Bi. Hellen
Kituo cha msaada wa Kisheria na haki za binadamu (LHRC), kilianzishwa Septemba 25, 1995 lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo Watanzania namna ya kulinda na kutetea haki zao.
Leave a comment