Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Membe aitega CCM kugombea urais
Habari za SiasaTangulizi

Membe aitega CCM kugombea urais

Marehemu Bernard Membe enzi za uhai wake
Spread the love

WAZIRI wa zamani wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe amesema, anatamani kujipima ubavu na Rais John Pombe Magufuli katika kinyang’anyiro cha Urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Lindi … (endelea).

Membe amesema, yeye ndiye anayeweza kuufanya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 ukawa na msisimko huku akiwataka vijana wenye imani na naye kuendelea kuwa watulivu wakisubiri kuona nini kitaendelea.

Mwanasiasa huyo ametoka kauli hiyo jana Jumamosi tarehe 20 Juni 2020 akiwa mkoani Lindi ambalo alizungumza na wananchi kuhusu adhima yake ya kuwania Urais wa Tanzania.

Hata hivyo, Membe ameonyesha wasiwasi kama hilo litawezekana kutokana na kile kilichofanywa na kikao cha Kamati Kuu ya CCM kutangaza kumvua uanachama.

Uamuzi huo ulitangaza mbele ya vyombo vya habari tarehe 28 Februari 2020 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kwa kile alichosema, Membe amekuwa hana mwenendo mzuri ndani ya chama hicho tangu mwaka 2014.

Alisema, Membe amekuwa akionyesha mwenendo ambao si mzuri licha ya kupewa adhabu ambazo zililenga kumsaidia ajirekebishe.

Hata hivyo, Dk. Bashiru Ally aliwahi kunukuliwa akisema, hayo ni mapendekezo ya kamati kuu ambayo watayawasilisha katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kwa uamuzi wa mwisho wa kuyaridhia kufukuzwa au kubatirisha.

Dk. Bashiru alisema kikao cha Halmashauri Kuu iliyokutana tarehe 13 Desemba 2019 jijini Mwanza chini ya Mwenyekiti, Rais Magufuli iliazimia kumwita na kumhoji Membe na wanachama wengine kwa ukiukwaji wa maadili.

Katibu mkuu huyo alisema, uamuzi wa mwisho utafanywa na kiko hicho pindi kitakapokutana.

Wakati uamuzi huo ukisubiriwa na mchakato wa uchukuaji wa fomu za Urais ukianza tarehe 15 hadi 30 Juni 2020, Membe ameibuka akionyesha kutaka kugombea Urais ndani ya chama hicho.

Membe aliyezaliwa tarehe 9 Novemba 1953, Rondo, Chiponda mkoani Lindi amesema, baada ya mchakato wa Urais ulipoanza, amesema alitumia karibu wiki nzima kutafakari, “sikuwa nimeamini kama kutakuwa na uchaguzi.”

Amesema, mambo mawili yalikuwa yanamfanya afikirie kutokuwapo kwa uchaguzi kwanza,”Tupo tayari kwenda katika uchaguzi kwa mazingira ya corona tuliyonayo.”

Pili, amesema,”Tupo tayari kwenda katika uchaguzi bila tume huru ya uchaguz,” ambayo itakuwa ngazi ya wilaya, mikoa na Taifa inayoshirikisha makundi yote?

Amesema, uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi utatoa haki kwa wote na kuondoa hofu kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi kutopeza nafasi zao endapo katika maeneo yao watashinda wagombea wa vyama vingine.

Membe amesema, “Lakini nikawa najiuliza, mwaka huu hakutakuwa na waangalizi wa kimataofa kwa sasa UNDP hawajatoa fedha, lakini suala la corona” na tunawezaje kwenda katika uchaguzi bila hawa waangalizi ambao watasema uchaguzi haukuwa huru, haki na amani au uchaguzi ulikuwa huru, haki na amani.

“Lakini kuna wanasiasa wakasema tukazanie hili la Tume. Ndio maana nimetumia wiki nzima iliyopita kutafakari ya tufanyeje,” amesema Membe, Mwanadiplomasia mashuhuri.

Membe amesema, wamefikiria kugombea ndani ya CCM na kufikia,”mwafaka kuwa sisi hatujamkosea mtu, sisi hatujawa waharifu, sisi hatujawa woga na tunajiamini na sisi tunaweza kugombea kabisa kwa sababu tu tunalindwa na katiba na siyo tamaduni.”

“Sisi tunaheshiku uamuzi wa Kamati Kuu, mwenyekiti wake, lakini kamati kuu isime kuwa sisi tulichokifanya ni mapendekezo tu na uamuzi utakwenda kufanya na mkutano wa Halmashauri kuu itakayokutana mwezi ujao wa saba.”

“Kama kamati kuu itasema ilichotamka ni makosa nje ya utaratibu, wakosema alichokisema Membe ni sahihi na shughuli za urais zipo sasa, sasa hivi Membe yuko huru kugombea, kujipima na Rais, wakitamka hivyo, kesho Jumatatu nitajaza fomu ya kugombda urais,” amesema Membe huku akishangiliwa na wananchi waliokuwa wakimsikiliza

“Lakini kama kamati kuu ikibaki na msimamo wake, huwezi kunituma niende Dodoma, nikikataliwa kupewa fomu, nikipewa hiyo fomu nikaenda mikoani na nisipowakuta kuwa wameitwa Dodoma, haitawezekana,” amesema

Akiendelea kuzungumza kwa umakini, Membe amesema,”Kwa hiyo, kugombea kwetu ndani ya CCM, na kuwa na msisimko kama Zanzibar, mnogeshaji ni mimi.”

“Mimi sitakwenda Dodoma mpaka kamati kuu au mjumbe wa kamati kuu, katibu mkuu au katibu mwenzk akinieleza uko huru na tusipofanya hivyo tutaingia kwenye mitego. Kama hatutapata ridhaa tunakitakia kila la kheri chama katika uchaguzi huu,” amesema.

Membe aliwaeleza wananchi hao kuwa,”Uchaguzi ni Oktoba na huu ni mwezi wa sita, chochote kinaweza kutokea hapa katikati.”

Kauli hiyo iliibua shangwe na kuendelea kusema,”Sasa naomba vijana wote kwa jina la Mungu, mtulie, msilete ghasia yoyote, hatujui Mungu alichotupangia, naelewa jinsi mioyo yenu inavyowaka moto.”

“Lengo tuwe na uchaguzi huru na wengine sisi tutaendelea kusema ukweli kwani msema kweli ni mpenzi wa Mungu,” ameaema

Itakumbukwa, wakati CCM ikitangaza kumvua uanachama Membe, kamati kuu ya chama hicho ilitangaza makatibu wakuu wa zamani wa chama hicho, Yusuf Makamba kusamehewa na Abdulrahman Kinana akipewa karipio linalomweka chini ya uangalizi wa miezi 18 na hataruhusiwa kugombea nafasi yoyote.

Vigogo hao waliingia matatani baada ya sauti zao na za wanachama wengine watatu kusambaa katika mitandao ya kijamii zikizungumzia kuporomoka kwa chama hicho na uenyekiti wa Dk John Magufuli, hali iliyoibua mjadala mkali ndani na nje ya chama hicho tawala.

Wanachama hao ambao ni wabunge; Nape Nnauye (Mtama), Willium Ngeleja (Sengerema) na January Makamba (Bumbuli) wao walimwomba msamaha Rais Magufuli na akawasamehe na hata mkutano wa Halmashauri kuu ulipitisha msamaha kwao.

Tarehe 6 Februari 2020, Membe alihojiwa na kamati ndogo ya udhibiti wa nidhamu inayoongozwa na Makamu amwenyekiti Bara, Philip Mangula Makao Makuu ya CCM, Dodoma huku Kinana na Makamba wakihojiwa Februari 10, ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba Dar es Salaam.

Membe alisema miongoni mwa maswali aliyoulizwa mbele ya kamati hiyo ni kama ana mpango wa kugombea urais, “niliwajibu kwamba ndiyo nitagombea na nakwambia…ningegombea wala nilikuwa sitanii.”

Alipoulizwa iwapo bado ana mpango wa kugombea licha ya kufukuzwa uanachama, Membe alijibu, “ndoto huwa haifi.”

Membe alikuwa miongoni mwa makada 42 wa CCM waliochukua fomu ya kuwania urais ndani ya chama hicho kurithi mikoba ya Rais mataafu Jakaya Kikwete mwaka 2015 lakini alijikuta akianguka kwa kuishia tano bora na mshindi akawa Dk. John Pombe Magufuli.

Wengine walioingia tano bora ukimwacha Magufuli na Membe ni; January Makamba, Balozi Asha Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ally.

Tatu bora wakaingia; Magufuli, Migiro na Balozi Amina.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!