March 5, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Aweso amtumbua bosi Duwasa

Juma Aweso, Waziri wa Maji

Spread the love

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amemtumbua Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa), Mhandisi David Pallangyo akitaka apangiwa kazi nyingine. Anaripoti Brightnes Boaz…(endelea)

Aweso amechukua uamuzi huo leo Alhamisi tarehe 10 Desemba 2020 ikiwa ni siku moja imepita tangu alipoapishwa kuwa Waziri wa Maji na Rais wa Tanzania, John Magufuli jana Jumatano Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Uamuzi huo ameuchukua katika kikao chake na watumishi wa Duwasa akiwataka kuimarisha huduma ya upatikanaji maji katika jiji la Dodoma.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano ya wizara hiyo imesema, Aweso amemtaka Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga kumbadilisha kituo cha kazi Palangyo.

“Tunahitaji kufanya kazi kwa kasi kubwa ili kuboresha huduma ya maji katika jiji la Dodoma, hivyo tuongeze nguvu ya utendaji kazi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea,” amesema Aweso ambaye ni Mbunge wa Pangani jijini Tanga.

Waziri Aweso amewaomba watumishi wa Duwasa, lazima watumie taaluma na weledi wa fani zao kwa kushirikiana ili kuhakikisha huduma ya maji inaimarika zaidi.

Pia, amewapongeza Duwasa kwa kazi wanayoifanya na kuwataka kuongeza nguvu zaidi katika huduma kwa wateja na kuhakikisha huduma inawafikia wakazi wa Jiji la Dodoma kama inavyostahili katika maeneo yote.

Waziri huyo amezitaka taasisi zote zilizopo chini ya wizara ya maji kuchukua hatua ili kuimarisha huduma ya upatikanaji maji nchini na kufanya kazi kwa kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ili wananchi wapate huduma ya maji iliyo bora.

Kikao hicho kilichowakutanisha watumishi wa Duwasa, kimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga pamoja na Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Nadhifa Kemikimba.

error: Content is protected !!