Sunday , 2 April 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema wamshangaa Ndugai, wahoji ‘tunakwendaje mahakamani?’ 
Habari za SiasaTangulizi

Chadema wamshangaa Ndugai, wahoji ‘tunakwendaje mahakamani?’ 

John Mrema, Mkurugenzi wa Itikadi Uenezi na Mawasiliano Chadema
Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeshangazwa na kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuwa hana mamlaka ya kuwafukuza bungeni, Halima Mdee na wenzake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI Online, leo Alhamisi, tarehe 10 Desemba 2020, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema, ni “jambo la kusikitisha kwamba mtu anayesimamia chombo cha kutunga sheria, anashindwa kusimamia sheria.”

Mrema aliombwa na mwandishi wa habari hizi kupata kauli yake, kufuatia uamuzi wa Spika Ndugai, kuendelea kuwatambua Mdee na wenzake 19, ambao wamefutwa uanachama na Chadema.

Spika Ndugai alinukuliwa na vyombo vya habari, Jumanne iliyoita, 8 Desemba 2020 akisema, “Chadema kama kinamshida Mdee na wenzake, waende Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) au Mahakamani.”

          Soma zaidi:-

Alitoa kauli hiyo, wakati wa hafla ya kuwaapisha Dk. Dorothy Gwajima na Dk. Leonard Chamriho, walioteuliwa na Rais John Magufuli, kuwa wabunge wa Bunge la Muungano na baadaye kuwafanya kuwa mawaziri.

Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, iliyokutana chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe, tarehe 27 Novemba 2020, iliamua kwa kauli moja, kumuondoa kwenye nafasi yake ya uenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Mdee na kisha kumfuta uanachama.

Mdee na wenzake 18, walituhumiwa na kupatikana na makosa ya utovu wa nidhamu na usaliti, ikiwamo kuhujumu chama, upendeleo, kutengeneza migogoro ndani ya chama; kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama, kughushi nyaraka za chama na kwenda bungeni kujiapisha, kinyume na maekelezo na maamuzi ya chama.

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Wengine waliovuliwa nyadhifa zao na kufutwa uanachama kutokana na makosa hayo, ni waliokuwa wajumbe wa CC, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Nusrat Hanje; aliyekuwa katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Grace Tendega na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga.

Wengine, ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; aliyekuwa katibu mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambat; aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.

Katika orodha hiyo, yupo pia Ceciia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba,  Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Katika taarifa yake kwa umma, Chadema kilisema, iwapo wanachama wake hao 19, waliopachikwa jina la Covid 19, hawakuridhika na hatua hiyo, waweza kukata rufaa Baraza Kuu (BKT), ndani ya siku 30 tangu kutolewa uamuzi huo.

Mrema anasema, “Spika Ndugai hapaswi kukimbia wajibu wake wa kisheria. Anapaswa kusimamia Katiba ya Jamhuri ya Muungano na sheria za uchaguzi. Hapaswi kutenda kinyume na kiapo chake.”

Ameongeza, “Spika Ndugai anapaswa kulishughulikia suala hili, kama alivyofanya kwa Sophia Simba, alipofukuzwa uanachama na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wabunge 8 wa Chama Cha Wananchi (CUF).”

Anahoji: “…sisi tunakwendaje tume ya uchaguzi,” anaeleza Mrema na kufafanua, “sisi tumemjulisha yeye kuwa hawa si wanachama wetu na yeye anapaswa kutumia mamlaka yake ya Kikatiba, kuwajulisha NEC, kama ambavyo amewahi kufanya kwa Sophia Simba na kwale wabunge wa CUF.”

Freeman Mbowe, Mwenyekiti Chadema Taifa

Katika Bunge la 11 ambalo Ndugai pia alikuwa Spika, CCM ilimfukuza uanachama aliyekuwa mwenyekiti wake wa Jumiya ya Wanawake ya chama hicho (UWT), na kisha wakamjulisha Spika Ndugai ambaye naye aliijulisha NEC juu ya jambo hilo.

NEC mara baada ya kupokea taarifa ya Spika wa Bunge, ilitaarifu umma kuhusu jambo hilo na kusema, hatua za kutangaza mtu wa kujaza nafasi yake, zinaendelea kuchukuliwa kufuatana na sheria inavyoelekeza.

Aidha, CUF kilipowafukuza wanachama wake, wabunge wake hao nane, kilimjulisha Spika Ndugai. Naye mara baada ya kupokea barua hiyo, aliijulisha NEC na nafasi hizo zikajazwa na wabunge wengine.

Mrema anasema, “…sisi tufuate nini NEC au mahakamani? Kama tutakwenda mahakamni, tutakwenda kwa suala la kughushi saini; na au mambo mengine yahusuyo jambo hilo. Kwa sasa, ni wajibu wake, kutenda kwa mujibu wa Katiba inavyomuelekeza.”

Amesema, Chadema waliwasisha kwa Spika Ndugai barua inayomjulisha kuwa Mdee na wenzake wamevuliwa uanachama, 29 Novemba 2020 na “sheria inamtaka yeye amwandikie mwenyekiti wa NEC kuhusu nafasi hizo kuwa wazi.

“Hayo mamlaka yako kwake. Hayako kwetu. Atumie mamlaka hayo kwa kuwa ndio aliyokabidhiwa. Siyo sisi.”

Alipoulizwa iwapo Mdee na wenzake, wamekwisha wasilisha rufaa zao, Mrema amesema, “mpaka leo, hatujapokea rufaa hata ya mtu mmoja. Lakini kwa mujibu wa katiba yetu (Chadema), wana siku 30 za kutaka rufaa na kwa sababu adhabu ilitolewa tarehe 27 Novemba, bado wana muda na wanaweza kuwasilisha rufaa hata siku ya mwisho.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia apangua mawaziri

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la...

Habari za Siasa

RC mstaafu afariki dunia, CCM yamlilia

Spread the loveALIYEWAHI kuwa mkuu wa mikoa ya Dodoma, Mara, Mtwara na...

Habari za Siasa

Marekani kuwekeza Dola 500 Mil kupeleka bidhaa na huduma Tanzania

Spread the loveMAKAMU wa Rais wa Marekani, Kamala Harris amesema miongoni mwa...

Habari za Siasa

Kamala ataja hatua mpya kuimarisha uhusiano wa kibiashara Tanzania, Marekani

Spread the loveKATIKA kuimaridha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya Tanzania...

error: Content is protected !!