Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto Kabwe, ‘azitoboa ’ Bajeti 5 za Rais Magufuli 
Habari za SiasaTangulizi

Zitto Kabwe, ‘azitoboa ’ Bajeti 5 za Rais Magufuli 

Spread the love

KIONGOZI wa chama cha siasa cha ACT- Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, amekosoa Bajeti kuu ya serikali na kusema, kila bajeti inapaswa kutafsiri maono, malengo na shabaha, ambazo hazijawahi kuonekana tangu Rais John Magufuli, kuingia madarakani.” Anaripoti Faki Sosi …(endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Jumapili, tarehe 14 Juni 2020, Zitto amesema, “tangu serikali ya Rais Magufuli, iingie madarakani, haijawahi kutimiza malengo yaliyowekwa katika bajeti zake.”

Ametoa kauli hiyo, siku tatu baada ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Philip Mpango, kuwasilisha mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya serikali katika mwaka wa fedha wa 2020/21.

Akichambua bajeti moja baada ya nyingine – kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2020/2021 – Zitto amesema, kila mwaka serikali imekuwa ikukusanya pungufu ya kile inachokikadiria.

Amesema, “katika bajeti ya kwanza ya Rais Magufuli (2016/2017), serikali serikali ilipanga kukusanya Sh. 29.5 trilioni. Lakini iliishia kukusanya kiasi cha Sh. 25.3 trilioni tu.

“Kushindwa kukusanya kwa kiwango hicho, kukafanya kutokufikia lengo la makusanyo hayo, kwa asilimia 14.33.Ukuzaji huu wa makisio kwa asilimia 31, ni mkubwa sana, ukulinganisha na wastani wa ukuzaji wa makisio ya bajeti wa asilimia 11 katika miaka miwili ya nyuma,” ameeleza.

Amesema, “Sababu kubwa ya serikali ya kushindwa kufikia malengo, ni kuweka makisio makubwa mno bila ushahidi wa takwimu za kutosha kuhusu hali ya uchumi wa nchi.

“Jambo hili lilisababisha ukamuaji mkubwa wa kodi kwa wafanyabishara, jambo ambalo lilisababisha biashara nyingi kufungwa, na hivyo kusababisha athari kubwa kwenye uchumi wa taifa hili.”

Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017, ilikuwa bajeti ya kwanza ya serikali ya Rais Magufuli.

“Licha ya serikali kutambua makosa yake haya ya kuweka makisio makubwa katika bajeti yake ya kwanza, bado haitaki kubadilika,” ameeleza.

Amesema, “kwa kuanza kushusha kasi ya kupandisha makisio kutoka asilimia 31 mpaka asilimia asilimia 7 mwaka 2017/18; asilimia 2 mwaka 2018/19, asilimia 2 mwaka  2019/2020 na asilimia 4 mwaka 2020/2021, tayari uchumi umeshaharibiwa kwa shughuli za uzalishaji kushuka na hivyo malengo ya makusanyo kuporomoka zaidi kuliko mwaka uliopita.”

Amesema, mwaka 2018/19 jumla ya Sh. 32.5 trilioni, zilitarajiwa kukusanywa, lakini kwa mujibu wa taarifa ya CAG, serikali ilikusanya Sh. 25.8 trilioni pekee na hivyo kutofikia lengo la makusanyo kwa asilimia 21.

Amesema, “mwaka 2019/20 jumla ya Sh. 33.1 trilioni, zilitarajiwa kukusanywa, lakini kwa mujibu wa taarifa ya Dk. Mpango, mpaka Aprili mwaka huu, makusanyo yamefikia Sh. 24.85 trilioni tu, ikiwa imebakia miezi 2 kabla ya mwaka wa fedha kuisha.”

Anasema, mpaka Aprili 2020, lengo la mapato ya kibajeti, halijafikiwa kwa asilimia 25 na kwamba makusanyo ya mapato yote ya serikali katika mwaka 2018/19, yalikuwa madogo kuliko bajeti ya mwaka uliotangulia wa 2017/18.

Kwenye uchambuzi wake huo Zitto anasema, kwa mujibu wa taarifa ya Mwaka ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Kamati ya Bunge ya Bajeti, licha ya makadiro na makusanyo halisi yaliyotarajiwa, utekelezaji wa bajeti uko chini ya asilimia 70.

Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini, ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2016/17, bajeti ya serikali ilitekelezwa kwa asilimia 66.5, mwaka 2017/18, asilimia 64.5, mwaka 2018/19 asilimia 68.6 na 2019/2020, ilitekelezwa kwa asilimia 62 pekee.

“Kwa ujumla bajeti zote tano za Serikali ya Awamu ya Tano, baada ya hii ya mwaka 2020/2021 kupitishwa na Bunge, zitakuwa ni jumla ya Sh. 162 trilioni. Je, fedha hizi zinaendana na hali halisi ya maendeleo ya wananchi,” amehoji Zitto.

Amesema, taarifa ya hali ya uchumi wa taifa 2019 iliyotolewa na Dk. Mpango, tarehe 11 Juni 2020, inaonyesha kuwa pato la taifa (GDP) limekua kwa asilimia 7, kama ilivyokuwa kwa mwaka 2018.

Hii maana yake ni kwamba, ukuaji wa uchumi haukuongezeka; bali ulibaki pale pale katika viwango vya mwaka uliopita.

Mwanasiasa huyo kijana amesema, katika miaka hiyo mitano ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), serikali imeshindwa kutumia rasilimali fedha za nchi kuchochea maendeleo kwa wananchi wake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!