Sunday , 3 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Urais Chadema: Nyalandu kutekeleza mambo 26 akiwa Rais 
Habari za SiasaTangulizi

Urais Chadema: Nyalandu kutekeleza mambo 26 akiwa Rais 

Lazaro Nyalandu
Spread the love

LAZARO Nyalandu, ametangaza kutia nia ya kugombea Urais wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku akibainisha vipaumbele 26 atakavyovifanya ndani ya siku 100 endapo atapewa ridhaa na Watanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Nyalandu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (Chadema) kanda ya Kati ametangaza nia hiyo leo Jumapili tarehe 14 Juni 2020 mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo anakuwa wa nne kujitosa katika kinyang’anyiro hicho kinachohitimishwa kesho Jumatatu tarehe 15 Juni 2020 cha wanaotaka kutia nia kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa Chadema.

Wengine waliokwisha tia nia ni, Dk. Maryrose Majige, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara na Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Katika hotuba yake, Nyalandu amesema,  leo, “nimemwandikia burua Katibu Mkuu wa nikimjulisha kusudio langu la kutia nia katika kinyang’anyiro cha kuwa Mgombea Urais kupitia CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2020..”

“Nasimama mbele yenu na mbele ya umma wa Watanzania, huku moyo wangu ukiwa umejaa shauku kubwa nikitamani kuiona Tanzania, nchi tuipendayo kwa moyo wote inapata ustawi na kuendeleza matamanio, matarajiona ndotoza watu wake.”

“Katika kuwapatia maendeleo endevu likiwa ni Taifa linalosimamia uhuru na  haki za watu, utawala wa sheria, uhuru wa vyombo vya habari,na demokrasia ya kweliinayowapa wananchi mamlaka ya juu kuhusu mustakadhi na mwelekeo ya nchi kupitia chagua zilizo huru na za haki,” amesema Nyalandu

Amesema, “Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliamini katika ulazima wa kuwaunganisha wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili waishi katika udugu, umoja, usawa, na mshikamano katika Taifa lililo huru na lenye amani, na kuifanya Tanzania kuwa kitivo cha amani na shauku ya wengi barani Afrika na ulimwenguni pote.”

Julius Nyerere, Hayati Baba wa Taifa

Nyalandu amesema, wakati Tanganyika inapata uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza mwaka 1961, Baba wa Taifa alisema ‘Tuwashe Mwenge, na tukauwe Kilimanjaro, ili uangaze ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.

Palipo na chuki kukawe na furaha, palipo na giza kukawe na nuru”.  Hii ndio asili ya Tanzania na hii ndio inayopaswa kuwa daima ya Tanzania.

“Watanzania wana matamanio na ndoto za maendeleo, vijana wao wana vipaji lukuki na wamejawa na uthubutu katika kutafuta maisha na kujiendeleza, huku  wakiamini katika ahadi ya ukuu wa Taifa lao, na uwepo wa amani tuliyo nayo tangu uhuru,” amesema

“Watanzania wanaamini katika kujenga jamii ya watu huru na wenye ushujaa, huku wakizifuata fursa za kujiendeleza kiuchumi na  kukabiliana na changamoto za maisha yao.”

Nyalandu aliyewahi kuwa waziri wa maliasili na utalii enzi za utawala wa awamu ya nne wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema,”Taifa letu likiwa bado changa, kwa minajili ya miaka tokea uhuru wake, na kwa sababu ya kuwa Taifa lenye vijana wengi, tuna ulazima wa kusimama pamoja kurejesha tena ndoto zilizo terereka na  matumaini yaliyopotea kuhusu ustawi wa maisha yetu ya sasa na kesho yetu.”

“Na kuhakikisha tunahuisha  tena matarajio na matamanio tuliyoyaamini tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” amesema.

Nyalandu aliyeokuwa Mbunge wa Singida Kaskazini tangu mwaka 2000 hadi tarehe 30 Oktoba 2017 kupitia CCM na kutangaza kujiunga Chadema, amesema,”Naamini katika kuiongoza Tanzania na watu wake ili kwa pamoja tuweze kuzifikia ndoto zetu.”

“Na tuweze kuhuisha tena imani na marajio ya kila mwananchi wetu katika kipindi ambacho uchumi wa mtu mmoja moja umedondoka, ugumu wa maisha umekithiri katika jamii, na simanzi la kutokujiamini limetanda katika nyuso za wengi huku kukiwa na mashaka na sintofamu kuhusu kesho yetu,” amesema

Amesema, kama ilivyoandikwa katika vitabu, “yeye aliye mnyonge na aseme mimi ni nina nguvu!”, naam,  Aliye maskini na aseme, Mimi ni tajiri!”.

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

“Kwa kuwa, kwa umoja wetu, na kwa kuthubutu kwetu, kupitia Uchaguzi Mkuu  wa Oktoba 2020, tunaweza kubadili mwelekeo wetu na kuirejesha tena Tanzania yenye fanaka, heri, na amani ya moyo kwa kila mtanzania.”

“Kwa pamoja, tuna uwezo wa kuuambia mlima huu ung’oke na ukatupwe bahari. Tunaweza, kwa pamoja, ifikapo Oktoba 2020, kutumia maji na kunikuyaivisha mawe, ili historia iandikwe juu ya uthubutu wa kizazi chetu,” amesema

Nyalandu amesema, kwa kuwa wahenga walisema kizazi chenye adili kitabarikiwa. Katika kipindi na majira haya, hata aliyemnyonge na asimame, sote tuvae uthubutu wa kurejesha upya U-Tanzania wetu katika ubora wake,

Amewema, kwa kuwa Tanzania yenye neema ya daimandiyo yalikuwa maono ya Mwasisi wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliposema “Ili tuendelee, tunahitaji watu, siasa safi, na uongozi bora”.

“Katika majira na nyakati kama hizi, changamoto na adui mkubwa anayetukabili sasa kama ni Taifa ni hofuiliyotanda miongoni mwa wanajamii na kwa pamoja tunaweza kusimama kama nchi na kuishinda hii hofu,” amesema Nyalandu

Amesema, “vijana waliomaliza masomo na kukosa ajira, chaguzi zilizofanyika bila kufuata misingi ya haki na demokrasia katika kuwapata baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa, huku watu wengi wakiwa na mashaka kama chaguzi zijazo zitakuwa huru na za haki, hofu ya kutokuwa na kipato cha kulisha familia na kusomesha watoto.”

Nyalandu ambaye mwaka 2015 alikuwa kati ya makada 48 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliojitosa kuwania urais ndani ya chama hicho na Dk. John Pombe Magufuli kuibuka mshindi amesema,”Hofu kwamba haki inaweza isitendeke endapo mwananchi ana shauri mahakamani. Hofu juu ya uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari na uandishi, na hofu ya kujieleza na kujiunga na vikundi vya kisiasa ama kijamii kwa utashi wa mtu binafsi.”

Jaji,Joseph Warioba, Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba

“Sote tunashuhudia uwepo wa hofu kubwa  miongoni mwa jamii, na ni sharti tusimame kama mashujaa wa kizazi chetu na kuishinda hofu.” Amesema

Nyalandu amesema, katika wakati wa utawala wake, Rais mataafu Benjamni Mkapa aliamini katika ushindani wa kisiasa na kuongoza serikali ambayo kauli mbiu yake ilikuwa uwazi naukweli.

Aliwahimiza watanzania kuhusu nidhamu ya kujenga uchumi na taasisi endelevu katika Taifa na kupambana na deni la Taifa na mfumuko wa bei.

Katika awamu ya nne ya Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, tulishuhudia kuongezeka kwa wigo na fursa za demokrasia, ikiwa ni pamoja na wanawake wengi zaidi kupata nafasi za uongozi katika siasa na sehemu nyeti za maamuzi Tanzania.

Amesema, katika awamu ya nne, tulishuhudia kupanuka kwa wigo wa demokrasia huku vyama vya upinzania vikiongeza viti vyao katika Bunge la Tanzania.

Katika kauli mbiu yake ya Ari Mpya na Kasi Mpya, Rais Kikwete aliweza kuiongezea Tanzania heshima kubwa katika Nyanja za mahusiano ya Kimataifa.

“Awamu ya sita chini ya uongozi wangu itaenzi misingi bora iliyojengwa na waasisi na viongozi waliotangulia huku ikiimarisha mifumo na taasisi za kuongoza nchi kupitia utawala thabiti wa sheria ambako mihimili ya serikali, Bunge na Mahamaka zitakuwa huru na kuwepo kwa uthibiti na uhakikikatika kuongoza nchi, kutungua sheria, na kusimamia utoaji haki kwa wote,” amesema

Nyalandu amesema, endapo Chama changu kitaniteua kuwa Mgombea na watanzania wakanipa ridhaa ya kuongoza Taifa, serikali nitakayoiongoza itatarajia kujikita katika kutekeleza mambo yafuata katika siku 100 za kwanza za uongozi wangu:- baadhi ya mambo hayo 25 ni

1. Tutarekebisha sheria ya ardhi kuruhusu wananchi kumiliki ardhi bila ukomo (Freehold lease) na kuwapimia wananchi maeneo ya ardhi kote nchini ili kurasimisha utajiri wa watanzania wote kupitia ardhi tunayoimiliki.

Hatua hii italeta ukomo kwa serikali kuu kupitia Rais wa nchi kuwa mmiliki wa ardhi ya watanzania, jambo linalowafanya wananchi wote kuwa wapangaji katika nchi yao wenyewe.

Aidha, hati zote za umiliki ardhi zitakuwa na thamani katika mabenki na amani za kifedha na kumwezesha mwananchi wa kawaidi kukopesheka na kuwa na mali isiyohamishika.

2. Kwa kuwa wajibu wa kiongozi mkuu  wa nchi kuhakisha watu wake wanao ulinzi na usalama, na kwamba wanaweze kumudu kujikimu kimaisha, nitahakikisha tunafanya kila linalowezekana kuongeza ajira kwa vijana na watanzania kwa ujumla, huku sekta binafsi ikiwa kipaumbele kama sekta kiongozi kwenye upatikanaji wa ajira nchini.

3. Tutaanza mara moja kuipitia upya rasimu ya Katiba Mpya ya Tanzania, kwa kuanzia na rasimu ya Jaji Warioba.

4. Tutairekebisha sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA ili iwe taasisi inayojitegemea na isiyolalamikiwa kuhusu uendeshaji wake au kuingiliwa kisiasa.

Hatua hii itahusisha pia kupunguza utitiri wa kodi, na kuwa na mfumo wa kodi ulio wazi na wa kueleweka kwa lengo la kupanua wigo wa walipa kodi na kuongeza mapato ya serikali kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

5. Tutaweka sera mpya itakayosimama sekta ya kilimo na uvuvi, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa pembejeo, uhakika wa masoko, kilimo cha umwagiliaji, na kuboresha shughuli za uvuvi katika maziwa na bahari kuu kwa lengo la kuwanufaisha wavuvi wadogo wadogo na kuthibiti wizi wa raslimali zetu katika bahari kuu.

6. Tutaipitia upya na kuirekebisha sheria ya Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB) kwa lengo la kuwaondolea wanafunzi faini za malimbikizo, na kuondoa ulazima wa kuanza kurejesha mkopo kabla ya mwanafunzi husika kupata ajira.

Aidha, tutarekebisha na kupunguza kiwango cha asilimia ya marejesho anayopaswa kuyafanya mwanafunzi ili kumpa unafuu wa kumudu maisha kwa kuongeza muda wa malipo.

7. Tutaweka sera mpya kuongoza sekta ya afya na kuinua kiwango cha utoaji huduma ya kitabibu nchini. Tupitia upya mpango wa Taifa wa upatikanaji wa maji safi na salama vijijini, na mijini.

8. Tutatunga sera mpya na wezeshi ili kufufua sekta ya mafuta na gesi na kuruhusu uwekezaji wa mitaji mikubwa-FDIs, na kuruhusu serikali kuhodhi asilimia ya hisa kwa niaba ya wananchi wa Tanzania.

Hatua hii itawezesha kuanzishwa Liquidified Natural Gas Plant-LNG katika ukanda wa Mtwara na kuifanya Tanzania kuwa nchi kiongozi katika uzalishaji wa gesi asilia na mafuta katika ukanda wa Afrika mashariki na SADC.

Hatua hii pia itahusisha kuihusha sekta ya madini iwafaidishe wachimbaji wadogo wadogo na kuruhusu uingizwaji wa mitaji mikubwa katika sekta hii, ikiwepo dhahabu, tanzanite, graphite, na urani.

9. Tutaimarisha mahusiano ya kikanda kwa kuidhinisha itifaki ya Afrika Mashariki kuhusu ‘Free Movement of persons, goods and services”, na ushirikiano wa ulinzi na usalama-Mutual Defense Pact, na kuongeza ushirikiano wa mafunzo katika kuimarisha Majeshi yetu ukanda wa Afrika Mashariki.

10. Tutarejea upya makubaliano ya biashara kati ya ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya-EPA, na kuidhinisha ushirikiano wenye maslahi kwa wafanyabiashara wa Tanzania hasa kwa fursa ya kuuza bidhaa zetu bila kodi katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.

11. Tutaingia mara moja kwenye “Bilateral Negotiation” kwa mkataba mpya wa kibiashara kati ya Tanzania na United Kingdom, kwa kuwa UK sio tena mwanachama wa EU.

12. Tutaongeza idadi ya nchi ambazo Watanzania wanaweza kusafiri bila ulazima wa kuwa na visa (visa free) kupitia makubalino baina ya nchi na nchi na kwa kuzingatia utaratibu wa kidiplomasia wa “resprocity”.

Hatua hii itaongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini, na itawawezesha Watanzania kusafiri kwa shughuli za kibiashara au vinginevyo katika mataifa mengi na kuiletea heshima pasipoti ya Tanzania.

13. Tutaweka sera ya kudumu ya kuimarisha utayari wa Majeshi ya ulinzi na usalama katika kuilinda chi yetu dhidi ya maadui na kulifanya Jeshi la Wanachi wa Tanzania (JWTZ) liendelee kuwa la kisasa Zaidi.

14. Tutatunga sheria kuruhusu ‘Dual Nationality”, ambako Mtanzania yeyote anayekubali uraia wa nchi nyingine hawezi kunyang’anywa haki ya Utanzania wake.

Hatua hii itawasaidia Watanzania waliopo nchi za nje kuweza kuendelea kuwekeza kiuchumi katika nchi yetu na kuongeza pato la Taifa huku tukiendelea kuhakikisha kila mtanzania anabaki kuwa raia wa Tanzania.

15. Tutaruhusu shughuli zote za kisiasa kutoka kwa vyama vya upinzani na wanaharati katika kukusanyika na kuwa na uhuru wa kuikosoa serikali.

Hatua hii itaongeza wigo wa demokrasia na kuvipa vyama vya upinzani nafasi ya kujiandaa kisera na kimuundo kwa ajili ya uchaguzi unaofuata.

16. Tutarekebisha sheria ya Habari ili kuruhusu uhuru kamili wa vyombo vya habari, na uhuru kamili wa wanahabari (reporters), ikiwa ni pamoja na  haki ya kulinda vyanzo vya habari kama nguzo muhimu kwa upatikanaji wa habari.

Waandishi wa Habari

17. Tutarejesha Bunge live.

18. Tutaendeleza uhuru uliopo wa kuabudu, na kuweka zuio la kudumu ili kusiwe na tozo za kodi kwa mashirika ya dini, na taasisi za kiraia ili ziendelee kushiriki kama wadau wa maendeleo nchini.

19. Tutaruhuru vyombo vya usafirishaji vyote (Mabasi, malori, meli, ndege, nk) kuwa huru kufanya safari zao usiku na mchana. Hatua hii itaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

20. Tutaboresha sekta ya elimu nchini, na kupitia upya haki na stahiki za walimu, kuanzia kupandishwa madaraja na mishahara, haki ya kupata uhamisho kujiunga na familia kwa wale waliioa au kuolewa, na malimbikizo ya mishahara kwa ngazi zote za elimu ya umma nchini.

21. Tutaimarisha uhifadhi, na kuongeza utalii nchini kwa kurekebisha mifumo ya kodi, tozo, mitaji, rasilimali watu, masoko, na uendeshaji wa sekta hii.

22. Tutaimarisha ushiriki wa Tanzania katika jitihada za kimataifa za kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi na athari zinazotarajiwa kulikumba eneo la Ikweta, ambako nchi yetu ipo.

23. Tutaimarisha ushiriki wa Tanzania katika Taasisi ya Kimataifa na kuimarisha mahusiano na ushirikiano wa kikanda, na kimataifa, na kuongeza nguvu ya diplomasia ya Tanzania katika Nyanja za kiuchumi, kisiasi, kiulinzi, na kijamii.

“Taifa letu linahitaji mabadiliko, na saa ya ukombozi imefika. Ungana nami (kupitia tovuti yangu lazaronyalandu.com) katika safari ya kuleta tumaini jipya kwa Watanzania. Sote tunaowajibu kwa nchi yetu,” amesema Nyalandu.

2 Comments

  • Acheni bwana hakuna lolote upinzani jipya la kuzidi awamu ya tano, mngekaa mjipange 2025 hapo ningewaelewa sio sasa jameni. Mtapewa kura ndio na wale wajinga na malimbukeni wasiojua nini maana ya maendeleo na siasa bora ndani ya serikali iliyopo. Yoyote mwenye uchungu na hamu ya kuona Tanzania inasonga mbele kamwe hata chagua yoyote zaidi ya CCM ya sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

20 wafariki dunia kwa mafuriko Manyara

Spread the loveMVUA za vuli zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zimeleta madhara...

Habari za Siasa

Dk. Biteko aagiza wakurugenzi TANESCO kukemea rushwa kwenye maeneo yao

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Uongozi wa Samia kuendelea hadi 2030

Spread the loveKWETU sisi tuliowahi kusoma sekondari, iwe O levo au A...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Bado askari wastaafu wanaonewa

Spread the loveRAIS wangu Samia Suluhu Hassan tunaendelea kumshukuru Mungu kwamba wote...

error: Content is protected !!