October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mch. Msigwa: Nina dhamira ya kweli ya urais

Mchungaji Peter Msigwa

Spread the love

MCHUNGAJI Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini ametangaza nia ya kuwania urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na kwamba ana dhamira ya kweli kuling’oa Taifa katika umasikini uliotopea. Anaandika Hamis Mguta, Dar es Salaam…(endelea).

Katika hotuba yake kwa wananchi aliyoitoa leo tarehe 14 Juni 2020, Msigwa amesema tayari amewasilisha taarifa rasmi ya kuomba kuteuliwa na chama chake, kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mpaka sasa, Msigwa atachuana na Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, kuteuliwa kupitushwa ili kugombea urais kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2020.

Mbunge huyo wa Iringa amesema, anataka kuongoza mageuzi makubwa ya kiutawala, kiuchumi na kielimu yatakayoleta maendeleo makubwa na ya haraka, yaliyo jumuishi na endelevu kwa manufaa ya sasa na yajayo ya Tanzania.

“Viongozi makini huota. Viongozi bora hubeba maono ya aina ya nchi wanayokusudia kuijenga. Ndoto yangu ni kuitoa Tanzania katika orodha ya nchi masikini sana duniani na kuipa mwelekeo sahihi wa kifikra, kiutawala na kisera utakaoiwezesha kuja kuwa miongoni mwa nchi zenye maendeleo makubwa kabisa duniani.

“Ninayo dhamira ya kweli, maono sahihi na uwezo wa kutosha wa kuiongoza vema Tanzania ili kuifikia ndoto hii kubwa. Naam, ndoto ya Tanzania yenye maendeleo ya uhakika!” amesema.

Amesema, serikali ya Rais John Magufuli imeendelea kujivunia ukuaji uchumi ule ule wa asilimia saba, ambao umekuwapo kwa zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Na kwamba, licha ya majivuno hayo, miaka 59 baada ya Uhuru, wanawake wengi wajawazito na watoto wanapoteza maisha kila siku kwasababu ya huduma duni za afya.

“Bado wananchi wengi wa vijijini wanatembea umbali mrefu kutafuta maji ya kunywa na ya kutumia majumbani mwao. Bado maelfu ya vijana wa Kitanzania hawana ajira wala matumaini ya kuwawezesha kumudu maisha yao.

“Hakuna jipya tena ambalo serikali ya CCM inaweza kufanya katika nchi hii likafanikiwa. Uzoefu wa CCM ni kushindwa. Umahiri wa CCM ni kutoa ahadi hewa na kushindwa kuzitekeleza.

“Udhaifu wa CCM ni kukosa dira na mwelekeo sahihi wa kushughulikia maendeleo ya nchi yetu. Uwezo wa CCM umeishia kwenye kushughulikia matatizo na kero ndogo-ndogo ambazo hata baada ya kutatuliwa kwake bado hakuifanyi nchi yetu kuwa na maendeleo makubwa,” amesema.

Msigwa amesema, miaka 59 baada ya Uhuru, Tanzania haihitaji serikali inayohangaika na kero na matatizo madogo-madogo ya kila siku.

“Hatuhitaji tena Rais wa kuhesabu matundu ya vyoo yaliyojengwa na serikali yake na kutueleza jinsi tulivyoendelea. Hatuhitaji Rais wa kuweka mawe ya msingi ya ujenzi wa madaraja…,tunahitaji Rais wa kufanya mageuzi na mapinduzi makubwa ya kiutawala, kiuchumi na kielimu,” amesema.

Amesema, hakuna njia ya mkato katika kuyafikia maendeleo makubwa na ya kweli ya Taifa letu na kwamba, tofauti kuu iliyopo baina yetu na nchi nyingi zilizoendelea duniani si rangi wala fedha bali ni fikra.

“Taifa lolote lile duniani linalohitaji kupata maendeleo makubwa, ni sharti lifikirie kwanza kutanua fikra za watu wake. Katika muktadha huu, kufanya mapinduzi makubwa ya kielimu na kiteknolojia ndiyo kitakuwa kipaumbele cha kwanza na cha msingi cha serikali yangu,” amesema.

Akizungumzia utawala bora, Msigwa amesema, kukosekana kwa utawala bora na uwajibikaji, kumekwamisha kwa kiasi kikubwa jitihada nyingi za kusukuma maendeleo ya nchi.

“Mathalan, kilimo kinachoajiri Watanzania wengi kimepuuzwa na kuporomoka, si kwasababu serikali haina fedha za kutosha, bali kwasababu tu serikali imepuuza na kuacha kutoa zaidi ya asilimia 80 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kilimo.

“Aidha, bila ridhaa wala idhini ya Bunge, tumeshuhudia serikali ikielekeza fedha nyingi katika ununuzi wa ndege ambazo zingepaswa kuelekezwa katika vipaumbele vingine vya msingi na vya haraka zaidi vya maendeleo,” amesema.

Hivyo, amesema anakusudia kuiongoza nchi katika kufanya mageuzi makubwa ya kikatiba na ambayo, pamoja na mambo mengine, yatahakikisha tunakuwa na Mahakama, Bunge na Taasisi Huru ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa isiyoingiliwa na serikali katika shughuli wala maamuzi yake.

Amesema, mfumo wa uchumi unaofuatwa na serikali iliyoko madarakani, umepitwa na wakati na hauendani na mahitaji ya dunia ya sasa.

Na kwamba, ni mfumo unaodhibitiwa zaidi na serikali na ambao umeua nguvu ya soko katika kuamua mustakabali wa uchumi.

“Matokeo ya mfumo wa uchumi uliopo sasa, ni Taifa kuingizwa katika mzigo mkubwa wa madeni na kushindwa kutengeneza ajira na fursa za maendeleo ya kiuchumi kwa watu.

“Iwapo serikali ya CCM itaachwa iendelee kuendesha uchumi wa nchi kwa namna ambavyo imekuwa ikifanya kwa miaka yote, nchi itakuwa masikini kupindukia kwa karne nyingi zaidi,” amesema.

Amesema, katika utawala wake anakusudia kuufumua kabisa mfumo wa uchumi uliopo na kuanzisha mfumo wa Uchumi wa Soko Jamii katika nchi yetu.

error: Content is protected !!