Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto avuna M/kiti, 120 Chadema Ubungo
Habari za Siasa

Zitto avuna M/kiti, 120 Chadema Ubungo

Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimevuna zaidi ya wanachama 120 kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa Wilaya ya Ubungo, Renatus Pamba. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Pamba na wenzake wamepokelewa na kukabidhiwa kadi ya chama hicho leo tarehe 15 Julai 2020, jijini Dar es Salaam na Mbarara Maharagande, Katibu wa Haki za Binadamu ACT-Wazalendo.

Akizungumza baada ya kupokelewa, Pamba amesema ameamua kujiunga na chama hicho baada ya kuridhishwa na kauli mbinu yake ya uzalendo kwanza akisema, mzalendo yoyote hulinda haki za wengine na maslahi ya Taifa.

“Ukiwa mzalendo lazima utalinda haki za wengine, kwa hiyo moyo wangu na wenzangu ukatafakari nikasema tukaongeze nguvu ACT ili tunapodai haki, tunamaanisha kutoka mioyoni mwetu,” amesema Pamba.

Amesema, yeye na wenzake ni waumini wa siasa safi na za kistaarabu, hivyo watafanya siasa safi kwa ajili ya kujenga ACT-Wazalendo wilayani Ubungo.

“Ubungo tutaenda kujenga chama kama tulivyojenga Chadema, tulikijenga kwa nguvu yetu tukiamini tuko pamoja na wenzetu, lakini sitaki kusema sana mwenye macho haambiwi tazama,” amesema Pamba.

Wakati huo huo, Pamba amezungumzia sababu zilizotajwa na Hemed Ally, Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, zilizopelekea yeye na wenzake kuvuliwa cheo.

Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu jana, Hemed amesema uongozi wa Chadema Ubungo ulivunjwa kutokana na viongozi wake kukiuka mwongozo wa uchaguzi. Pamba amesema, sababu hizo si za kweli.

“Nilivyoona wenzangu wanaondoka, nilijiuliza kwa nini wanaondoka. Nikatafakari na mimi nikiondoka nitaambiwa nimenunuliwa na CCM au kibaraka wa mtu fulani. Nilisema jana. Nikasikia viongozi wanajibu, ulimi wa kweli utasema ukweli na uongo ni uongo,” amesema Pamba na kuongeza:

“Watu wanajua kipi cha ukweli na kipi cha uongo, leo hii tukianza kiwekeana ndimi za uongo tunaifanya siasa isikubalike ndani ya jamii.”

Akizungumzia mapokezi hayo, Maharagande amesema chama hicho kimewapokea wanachama hao, kwa kuwa ni haki yao ya kidemokrasia.

“Hii ni kawaida katika haki za demokrasia, hata sisi tulihama CUF kuja ACT-Wazalendo na mtu huhama kwa sababu. Hali hii inapaswa kuzoeleka. Hii kazi inaendelea na tunapanga usajili mkubwa sana,” amesema Maharagande.

Salum Sudi, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam amesema, wanachama hao wana haki ya kugombea kama wanachama wengine wa chama hicho.

“Hapa kwetu wote mnakua na haki ya kugombea kama wanachama wengine. Hapa hakuna muasisi wala mkubwa,” amesema Sudi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!