Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Waziri, Mbunge waparuana kisa Dodoma kuongoza kwa dhulma
Habari za Siasa

Waziri, Mbunge waparuana kisa Dodoma kuongoza kwa dhulma

Spread the love

 

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema mkoa wa Dodoma sasa ndio mkoa unaoongoza kitaifa kwa migogoro ya ardhi nchini.

Amesema migogoro hiyo imetokana na dhulma zilizofanywa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma ambayo baadaye ilikuwa jiji, Godwin Kunambi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Madai hayo yameibuka leo tarehe 21 Juni, 2022 bungeni jijini Dodoma, wakati Kunambi ambaye sasa ni Mbunge wa Mlimba (CCM) akichangia Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Kunambi ambaye alikuwa Mkurugenzi wa jiji hilo kuanzia tarehe 10 Septemba, 2016 hadi Agosti, 2020, amesema inashangaza kuona Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 60, ikiwa imetoa hati za umiliki wa ardhi kwa watu milioni mbili pekee tangu nchi ipate uhuru.

Amesema licha ya nchi jirani ya Kenya yenye idadi ya watu milioni 48, imefanikiwa kutoa hati hizo kwa watu milioni 11.

Akitumia mifano ya Baba wa Taifa, Kunambi amesema ili nchi yoyote iwe na maendeleo lazima iwe na watu, siasa safi na mwisho ardhi.

“Nchi yetu inakadiriwa kuwa na ardhi yenye kilomita za mraba 945,000, Kenya wana ardhi 580,000,” amesema.

Amesema kutokana na mwenendo huo wa kusuasua kutoa hati za ardhi kumesababisha serikali kukosa mapato kutokana na kodi mbalimbali zinazopatikana kwenye sekta ya ardhi.

Pia amesema hali hiyo imesababisha wakulima kuendelea kuwa maskini kwa kuwa ardhi walizonazo hazina thamani, hivyo hata hawakopesheki.

“Ardhi ni kila kitu, madini yapo kwenye ardhi, kilimo ni kwenye ardhi, waziri wa kilimo atakwama kwa sababu mkulima ana ardhi ambayo haina faida, haina thamani, hakopesheki, ardhi ili iwe na thamani lazima ipimwe,” amesema.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula

Aidha, ameongeza kuwa ili taratibu za upimaji wa ardhi kwa mujibu wa sheria zifanikiwe haraka lazima wizara husika ianze na mpango kabambe.

Amesema tangu Tanzania ipate uhuru halmashauri pekee iliyokuwa Mipango ya jumla ya kuendeleza miji (Master plan), ni Dodoma peke yake jambo ambalo Waziri Mabula alimsahihisha kuwa sasa Halmashauri 26 zina ‘Master plan’.

Ameendelea kushauri kuwa ili upimaji na utoaji huo wa hati uende haraka, wizara izingatie kuwa na mambo matatu ambayo mpango kabambe, ramani za mipango miji na ramani ya upimaji.

Mbunge huyo ametoa mfano kuwa alipokuwa mkurugenzi wa jiji Dodoma alitumia sekta binafsi kupima viwanja na kufanikiwa kutoa hati kwa viwanja 390,000.

Hata hivyo, Waziri Mabula alitoa taarifa kwa Naibu Spika Mussa Zungu kwamba mfano anaoutoa mbunge huyo ndiyo uliosababisha Dodoma kuipiku Kinondoni kwa migogoro ya viwanja.

“Ninaomba msemaji anapozungumza asitupe story ambazo sasa hivi ndio zinatuletea matatizo kwa nchi hii.

“Akiwa mkurugenzi wa Dodoma kama anavyosema tulikuwa na story ya Kinondoni kuongoza kwa migogoro, sasa hivi kitaifa Dodoma inaongoza kwa dhulma ambazo amezifanya kwa wananchi. Kwa hiyo huo sio mfano mzuri kwa maana ya mafanikio aliyoyafanya akiwa kama kiongozi,” amesema Mabula.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!