May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waraka wa corona wamponza Prof. Bisanda wa Chuo Kikuu

Profesa Elifas Bisanda, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)

Spread the love

WARAKA kuhusu tahadhari ya maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19), uliotolewa na Profesa Elifas Bisanda, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), umeikera Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Tayari wizara hiyo imempa onyo kwa Prof. Bisanda na kumsisitiza kwamba, aache kutumia nembo ya serikali kufikisha mawazo yake kwa jamii.

Tarehe 8 Februari 2021, Prof. Bisanda alitoa waraka huo akiuelekeza kwa wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho, akisema “ni budi kila mmoja wetu achukue tahadhari, kama inavyoelekezwa na viongozi wetu wa kitaifa.”

“Ugonjwa huu unaeleweka, hauna tiba katika mahospitali yetu. Hata nchi zilizoendelea kama Marekani na Uingereza zimeshindwa kuutibu. Chanjo inayopigiwa upatu, haijathibishwa kama inaweza kuuzuia,” anaeleza Prof. Bisanda.

Waraka huo, unaelekeza wanafunzi “wanaoingia chuoni, tunasisitiza kuwa wakae majumbani na kusoma kwa mtandao (online). Hatutaruhusu wanafunzi na wageni kuingia kwenye kampasi zetu bila sababu maalum, kama kuja kuchukua vyeti au kufanya “clearance.”

Hata hivyo, siku moja baadaye, Wizara ya Elimu ilitoa taarifa kwa umma, iliyosainiwa na Oliva Kato, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa wizara hiyo ikisema, tahadhari iliyotolewa kupitia waraka wa Profesa Bisanda ‘ni batili.’

“Maelekezo yaliyotolewa na Profesa Bisanda, ambayo ni maoni yake binafsi, hayakuzingatia mwongozo wa udhubiti wa maambukizi ya ugonjwa wa corona katika shule, vyuo na taasisi za elimu nchini wa Wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto wa tarehe 27 Mei 2020.”

Oliva anasema, wizara inaelekeza wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuendelea na masomo na kazi zao kama kawaida.

“Wizara inatoa rai kwa taasisi zote za elimu nchini, kuzingatia maelekezo ya serikali kuhusu udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa corona,” amesema na kuongeza;

“Vilevile, wizara inatoa onyo kwa viongozi na watumishi wa wizara ya elimu, sayansi na teknolojia pamoja na taasisi zake kuacha kutumia nembo za serikali wanapotoa maoni yao binafsi,” amesema.

Katika waraka wake Prof. Bisanda, ameandika “naandika hapa kwa uchungu sana, ninapohesabu watu ambao wamefariki katika siku chache zilizopita. Wasomi na wasio wasomi. Wazee na hata vijana. Tutaendelea kupuuzia maelekezo ya viongozi wetu hadi lini?”

Kuhusu kujisomea, makamu mkuu wa chuo hicho anasema “utaratibu ufanyike kuwasaidia wanaotaka kutumia maktaba kama ni lazima, wengi wanaitumia maktaba yetu kama mahali pa kujisomea tu. Maelekezo haya ni kwa ajili ya makao makuu, vituo vyote vya mikoa na vituo vya uratibu vilivyoko nchini.”

Mwisho wa waraka huo, Profesa Bisanda anasema “nimetoa maoni yangu, kama ushauri, nikiwa nawajibika pia kama kiongozi, kuwalinda wale wote ninaowaongoza. Asanteni sana, Mungu awalinde, tumalize huu mwaka salama.”

error: Content is protected !!