May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo ‘wamtesti’ Dk. Mwinyi

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Spread the love

 

CHAMA cha ACT- Wazalendo, kimemshauri Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kuunda “tume ya maridhiano” ili kutibu vidonda vya uchaguzi mkuu uliyopita, Visiwani Zanzibar. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

ACT-Wazalendo kimesema hayo leo Jumatano tarehe 10 Februari 2021, ikiwa ni zimetimia siku 100, tangu Rais Mwinyi alipoingia madarakani, baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 2020, visiwani humo.

Ombi hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alipoulizwa na MwanaHALISI Online maoni ya chama hicho kuhusu siku 100 za Dk. Mwinyi madarakani.

Dk. Mwinyi, aliapishwa tarehe 2 Novemba 2020, kuwa Rais wa Zanzibar akichukua nafasi ya Dk. Ali Mohamed Shein, aliyemaliza muda wake wa utawala wa miaka kumi kwa mujibu wa Katiba.

“Hili linataka tume maalumu ya maridhiano na maelewano ili kuanza upya, na si kukomoana, haya yanapaswa kutupiwa macho ili kuendeleza uongozi wa serikali yake,” amesema Ado.

Amesema, eneo la fidia kwa waathirika wa uchaguzi huo linahitaji msukumo mkubwa, kwa kuwa katika mchakato wake kuna baadhi ya watu walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa.

“Eneo pekee ambalo linahitaji msukumo zaidi kwa maoni yangu ni namna ya kushughulika na wahanga wa uchaguzi wa mwaka 2020, uchaguzi ambao umeacha makovu makubwa sana, uchaguzi ambao umechukua roho za watu, umeumiza wengi,” amesema Ado.

Ado amesisitiza kwamba, ili serikali ya Rais Mwinyi iwe na mwanzo mzuri, inabidi iwalipe fidia wahanga hao.

“Nadhani kuna muhimu sana serikali kuichukua hii kama ajenda, ili kuonesha kwamba kweli tunataka mwanzo mpya, kwa maana ya kuwafidia walioumizwa na waliofiwa,” amesema Ado.

Sambamba na kuwachukulia hatua waliohusika katika vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kabla na baada ya uchaguzi huo.

“…na kuchukua hatua kwa wale wataobainika kwamba walishiriki katika vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu,” amesema Ado.

Tarehe 19 Novemba 2020, wakati anatoa tathimini ya uchaguzi huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Sirro amesema watu wawili walifariki na kadhaa kujeruhiwa visiwani humo, katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Akizungumzia siku 100 za Rais Mwinyi baada ya kuapishwa tarehe 2 Novemba 2020 kuongoza Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ado amesema kiongozi huyo amepata mafanikio katika baadhi ya maeneo.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa na kuleta maridhiano na wapinzani.

Katika mapambano dhidi ya rushwa, Ado amesema Dk. Mwinyi amefanikiwa kuongeza jitihada za kutokomeza vitendo vya rushwa hasa katika taasisi za umma.

“Maeneo ambayo yamepiga hatua kubwa ni maeneo ya mapambano dhidi ya rushwa, Zanzibar ajenda ya rushwa haikuwa inatiliwa mkazo mkubwa kwa miaka mingi, tukisema mapambano ya rushwa na ufisadi tulizoea kusikia Bara,” amesema Ado.

Ado amesema “kulikuwa hakuna jitihada kubwa kwa upande wa Zanzibar, lakini Mwinyi amejipambanua kwa maana anasimamia mambo haya ya mapambano dhidi ya rushwa. Utaona hatua kubwa zimechukuliwa dhidi ya watendaji mbalimbali wa serikali bila kuangalia mtu usoni.”
Mwanasiasa huyo amemshauri, Dk. Mwinyi kuiongezea nguvu Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), ili kutokomeza kabisa rushwa visiwani humo.

“Hili ni eneo ambalo nadhani ataliendeleza hasa kwa kuipa nguvu na meno taasisi ya kupambana na rushwa ZAECA,” amesema Ado.

Akitaja eneo la pili ambalo Dk. Mwinyi amefanikiwa, Ado amesema kiongozi huyo ameleta umoja wa kitaifa kupitia maridhiano yake na chama kikuu cha upinzani nchini humo, ACT-Wazalendo.

“Eneo la pili ni kuhusu maridhiano, ametamka kwa kinywa chake maneno ambayo hata watangulizi wake hawakuyasema, amejipambanua waziwazi kwamba ni muumini wa maridhiano.

“Amekuwa na msisitizo wa wazi kwa wasaidizi wake kwamba wawahudumie Wazanzibari bila kujali itikadi zao au misimamo yao ya kisiasa,” amesema Ado.

Katibu huyo wa ACT-Wazalendo amesema awali, Zanzibar kulikuwa na mpasuko ambao ulisababisha ubaguzi katika utoaji huduma za kijamii na ajira.

“Kulikuwa na shida kubwa sana Zanzibar kwenye eneo hilo, hasa ajira na utoaji huduma mbalimbali, ni eneo ambalo Rais Mwinyi ameweka msingi ukiendelezwa unaweza ukawa na manufaa mazuri,” amesema Ado.

Ado ametaja eneo lingine la mafanikio kuwa ni “ni eneo la kuondokana na kufanya kazi kwa mazoea, kumekuwa na shida hiyo kwa baadhi ya huduma Zanzibar, watu hawafuati misingi ya kazi, hawawajibiki, Rais Mwinyi ameonesha anataka kuchukua hatua katika maeneo hayo,” amesema Ado.

Wakati akizungumza na wanahabari kuhusu mafanikio yake katika siku 100 za uongozi wake, jana Jumanne, tarehe 9 Februari 2021 visiwani Zanzibar, Dk. Mwinyi alisema, amefanikiwa kuleta umoja wa kitaifa, kudhibiti mianya ya rushwa pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato.

Kiongozi huyo wa Zanzibar, ameahidi kuitumia vyema ZAECA, katika kuwabana watu waliotafuna fedha za umma ili wazirudishe serikalini.

error: Content is protected !!