Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wagombea 127 wa udiwani kutoka vyama 18 kuchaguliwa kesho
Habari za Siasa

Wagombea 127 wa udiwani kutoka vyama 18 kuchaguliwa kesho

Wapiga kura
Spread the love

Wagombea udiwani 127 kutoka vyama 18 vya siasa wanatarajiwa kupigiwa kura katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 22 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 20 Machi 2024. Anaripoti Mwandishi wetu, Dar es Salaam… (endelea).

Hayo yabainishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa), Jacobs Mwambegele jijini Dar es Salaam wakati akitoa risala ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 22 za Tanzania Bara.

Jaji Mwambegele amesema kati ya wagombea hao 127 wagombea wanaume ni 89 na wanawake ni 38 na kuongeza kuwa wapiga kura 128,157 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, watashiriki katika uchaguzi huo mdogo na jumla ya vituo 373 vya kupigia kura vitatumika.

“Tume inatoa pongezi kwa wadau wote wakiwemo wapiga kura na wananchi katika kata 22 zenye uchaguzi kwa utulivu waliouonesha wakati wote wa kipindi cha kampeni,” amesema Jaji Mwambegele.

Jaji Mwambegele wasimamizi wa uchaguzi katika kata husika wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha mawakala wa vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi.

“Mawakala wanawajibika kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao na katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu za uchaguzi na Maelekezo ya Tume,” amefafanua Jaji Mwambegele.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa), Jacobs Mwambegele akizungumza jijini Dar es Salaam leo tarehe 19 Machi 2024 wakati akitoa Risala ya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 22 za Tanzania Bara.

Aliwataka wapiga kura katika uchaguzi huu mdogo, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura hapo kesho, ili kuwachagua viongozi wanaowataka huku akivikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wengine wa uchaguzi kujiepusha na vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.

“Mafanikio ya uchaguzi huu yatatokana na kuwepo kwa hali ya utulivu na amani katika maeneo yote yenye uchaguzi. Hivyo, Tume inatarajia kuona hali ya amani na utulivu iliyopo sasa inaendelea kuwepo hadi shughuli za uchaguzi zitakapokamilika,” aliongeza Jaji Mwambegele.

Alivikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala, wapiga kura na wananchi wote kwa ujumla kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 22, zinahitimishwa rasmi leo tarehe 19 Machi 2024, hivyo vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao hawatakiwi kufanya kampeni za aina yeyote zaidi ya saa 12:00 jioni ya leo.

Ametaja mambo mengine ambayo hayaruhusiwi kufanyika baada ya saa 12:00 na siku ya uchaguzi kuwa ni pamoja na kutumia alama za vyama vya siasa zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi na kwamba upigaji kura katika maeneo yote ya uchaguzi, utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Alikumbusha kuwa vituo vya Kupigia Kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa10:00 jioni. Iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura na mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00 jioni.

“Watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye kata husika na wana kadi zao za mpiga kura,” amesema.

Hata hivyo, amesema tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala kama vile, Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili mradi majina yaliyopo katika vitambulisho hivyo, yawe sawa na yaliyokuwepo katika kadi ya mpiga kura.

Jaji Mwambegele alieleza kuwa kutakuwa na majalada ya nukta nundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye uoni hafifu na wenye ulemavu wa kuona ili yawasaidie kupiga kura bila usaidizi na kwa wapiga kura wenye ulemavu wa kuona na ambao hawawezi kutumia majalada hayo, wataruhusiwa kwenda vituoni na watu ambao wanawaamini na ambao watawachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.

Kuhusu kipaumbele kwa wapiga kura, Jaji Mwambegele alisema katika vituo vya kupigia kura, kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaofika na watoto wao vituoni.

Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa maelekezo yaliyomo kwenye Maadili ya Uchaguzi ya Mwaka 2020, wapiga kura watatakiwa kuondoka vituoni mara tu baada ya kupiga kura. Hivyo, Tume inawashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.

Kata zinazofanya uchaguzi ni Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Mshikamano (Halmashauri ya Manispaa ya Musoma), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga), Fukayosi (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).

Kata nyingine ni Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu), Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za SiasaTangulizi

Samia awataka watanzania kudumisha muungano

Spread the loveRais wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuendeleza Muungano kwa...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

error: Content is protected !!