Mahakama ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imemhukumu kifungo cha miezi sita jela mwandishi wa habari wa Congo, Stanis Bujakera baada ya kukutwa na hatia ya kueneza habari za uongo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Wakili wa Bujakera, Jean-Marie Kabengela amesema jana Jumatatu majaji wametoa adhabu hiyo ya kifungo cha miezi sita pamoja na kulipa faini ya faranga milioni 1 za Congo sawa na Sh 940,000.
Aliongeza kuwa Bujakera, ambaye anafanya kazi katika vyombo vya habari vya kimataifa ikiwa ni pamoja na Jeune Afrique na Reuters, anatarajiwa kuondoka katika gereza ambalo amekuwa akishikiliwa tangu Septemba mwaka jana kwa sababu tayari ameshatumikia muda huo.
Wakili huyo alisema, kwa kuzingatia taratibu za kawaida katika kesi hizo, timu ya mawakili inayomwakilisha Bujakera itarejea tena mahakamani hapo leo Jumanne, kupata nakala ya uamuzi huo na kulipa faini hiyo ili aachiliwe.
Bujakera, ambaye amekana mashtaka yote, alikamatwa katika mji mkuu Kinshasa kwa tuhuma za kueneza habari za uongo kuhusu mauaji ya mwanasiasa mashuhuri wa upinzani katika makala iliyochapishwa na Jeune Afrique, gazeti la habari la Ufaransa limesema.
Mwendesha mashtaka katika kesi hiyo mapema mwezi huu alikuwa ameitaka mahakama ya Kinshasa kumhukumu Bujakera kifungo cha miaka 20 jela.
Mashirika ya haki za ndani na kimataifa yakiwemo Reporters Without Borders na Amnesty International yalilaani kuzuiliwa kwa Bujakera, na kuliita shambulio dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.
Leave a comment