SERIKALI imetakiwa kuwaongezea mamlaka wakaguzi wa ndani ili waweze kuzuia ubadhirifu na wizi wa mali ya umma unaofanywa na baadhi ya viongozi wa halmashauri nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Wito huo umetolewa leo tarehe 16 Februari 2024, bungeni jijini Dodoma, na baadhi ya wabunge ambao walidai kwa sasa wakaguzi hao hawana mamlaka ya kuwashughulikia viongozi wa halmashauri kwa kuwa ni wakubwa wao (maboss).
Mbunge Viti Maalum, Agnesta Lambart, akiuliza swali kwa niaba ya mwenzake, Nusrat Hanje, amehoji kwa nini Serikali isiwahamishe wakaguzi hao katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ili wawe huru katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Serikali ina mkakati gani wa kuwajengea uwezi wa kimamlaka wakaguzi wakuu wa ndani ili kuzuia ubadhirifu na wizi wa mali za umma?,” amesema Kaiza na kuongeza:
“Moja kati ya changamoto wanazokutana nazo wakaguzi wa ndani ni hili ambalo wao wanawakagua mabosi wao jambo ambalo linapelekea ufanisi katika utendaji wao wa kazi kuwa mdogo. Lini Serikali itawaondoia chini ya wakurugenzi wa serikali za mitaa ikibidi kuwapeleka chini ya CAG?”
Naye Mbunge wa Kondoa, Ally Makoa alisema “Wizara ya Fedha haioni haja kitengo hiki cha ukaguzi wa ndani kikaondolewa kwa mkurugenzi japo kikapelekwa kwa mkuu wa wilaya ili wawe huru zaidi?”
Akiwajibu wabunge hao, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, amesema wakaguzi hao hawawezi kuwa chini ya CAG kwa kuwa ni taasisi nyingine.
Amesema wakaguzi hao ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za serikali za kila kwa kukagua miradi kabla haijaanza, wakati wa kazi zinaendelea ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza. Wakati CAG ni taasisi inayokagua mradi wa serikali baada ya kukamilika ili kubaini mapungufu yaliyopo kwa ajili ya kuishauri Serikali hatua za kuchukua.
Leave a comment