Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge 11 watengwa Chadema
Habari za Siasa

Wabunge 11 watengwa Chadema

Spread the love

TAKRIBANI wabunge 11 kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameng’olewa kutoka kwenye group la WhatsApp la wabunge wa chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kuondolewa kwa wabunge hao kutoka katika group hilo ambalo hutumika kama sehemu ya mpango kazi wa kila siku wa wabunge wa Chadema, ni ishara ya kuwapa mkono wa kwaheri, kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa 25 Oktoba mwaka huu. 

Mtoa taarifa wa MwanaHALISI ameeleza kuwa wabunge hao waliondolewa kwa maelekezo ya viongozi wajuu wa wabunge wa Chadema.

Miongoni mwa viongozi waliomo kwenye group hilo la WhatsApp, ni pamoja na Freeman Mbowe, Kiongozi wa Upinzani bungeni na mwenyekiti wa chama hicho; Katibu Mkuu, John Mnyika; Naibu Katibu Bara, Benson Kigaila na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja tangu kuchukuliwa kwa hatua kama hiyo, Joseph Selasini, mbunge wa Chadema katika jimbo la Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Akilihutubia Bunge mjini Dodoma, Alhamisi iliyopita, Selasini aliliambia Bunge kuwa ametengwa na wabunge wenzake wa Chadema, ikiwamo kuondolewa bila kupewa taarifa, kwenye group la WhatsApp.”

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu, hatua ya kuondolewa kwa wabunge hao, kumetokana na uamuzi wao wa kukaidi maelekezo ya mwenyekiti wao, Freeman Mbowe ya kutaka kutohudhuria vikao vya Bunge.

Mbowe alielekeza wabunge wa Chadema kutohudhuria vikao vya Bunge kwa maelezo kuwa ndani ya ukumbi na viwanja vya Bunge, siyo eneo salama. Alisema eneo hilo limesheheni virusi vya Corona.

 

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika

Akataka wabunge wake, wajitenge na maeneo hayo kwa siku 14 ili kuangalia afya zao. Amri hiyo ya Mbowe inapingwa na wabunge wake kwa maelezo kuwa siyo shirikishi; na haiwatendei haki wananachi wanaowakilisha bungeni.

Wabunge waliondolewa kwenye group hilo, ni kama ifuatavyo: David Silinde, mbunge wa Momba, mkoani Songwe; Jafary Michael, mbunge wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro; Willifred Lwakate, mbunge wa Bukoba Mjini, mkoani Kagera na Latifa Chade, mbunge wa Viti Maalum mkoani Lindi.

Wengine waliokatishwa mawasiliano na chama na wabunge wenzao, ni Peter Lijualikali, mbunge wa Kilombero; Mariam Msabaha, mbunge wa Viti Maalum Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Sabrina Sungura, mbunge wa Viti Maalum kutokea mkoa wa Kigoma.

Katika orodha hiyo, wapo pia Suzana Masele, mbunge wa Viti Maalum kutokea mkoani Mwanza; Joyce Sokombi, mbunge wa Viti Maalum kutokea mkoani Mara; Mbunge wa Viti Maalum kutokea mkoani Mbeya, Risala Kabongo; mbunge wa Viti Maalum kutokea mkoani Manyara na Rose Kamil Slaa.

Wabunge wawili wa Chadema, Anthony Komu, Moshi Vijijini na Selasini, waliondolewa mara baada ya kutangaza kuwa katika uchaguzi ujao, hawatagombea majimbo yao ya sasa, kupitia Chadema. Walisema, watagombea kupitia NCCR- Mageuzi.

Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu

“Hawa tumewaondoa na hii ni salaam kuwa siyo wenzetu katika mapambano haya ya kudai haki,” ameeleza mmoja wa wabunge wa Chadema aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Amesema, pamoja na hatua hizo, wanatarajia kuwa chama chao kitawaita kuwahoji ili kuweza kuwapa adhabu kubwa zaidi, kwa wale ambao bado wataendelea kubaki Chadema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!