May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vurugu za familia chanzo watoto wa mitaani, Tunu Pinda atoa neno

Spread the love

 

MWENYEKITI wa kamati ya Dorcas iliyopo katika Kanisa la Upendo Revival Christian Center TAG, jijini Dodoma, Annie Maugo, amesema matatizo makubwa ya kuwepo kwa watoto wa mitaani ni kutokana na migogoro ya kifamilia. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Ameyasema hayo leo Jumamosi, tarehe 25 Desemba 2021, muda mfupi baada ya kumaliza ibada kuu na kuanza ibada maalum ya chakula cha pamoja na utoaji zawadi kwa na watoto yatima, wajane, watoto wa mitaani pamoja na wale waishio katika mazingira magumu.

Maugo amesema kamati hiyo ambayo iko chini ya kanisa hilo wamekuwa na utaratibu kula chakula na kutoa zawadi mbalimbali kwa watoto waliopo mashuleni na kutoa misaada mbalimbali kwa makundi hayo.

Amesema kwa siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo wameweza kutoa zawadi mbalimbali kwa makundi hayo ambapo gharama zote ni Sh.25 milioni.

 

Hata hivyo, Annie amesema kanisa limekuwa likihubiri neno la Mungu sambamba na kuwajali watu kimwili na Kiroho.

“Tumetoa vifaa mbalimbali vya masomo kwa wanafunzi wanaoingia shuleni Januari mwakani na pia tumetoa chakula, sabuni mafuta ya kula pamoja na mafuta ya kupaka.”

“Jumla ya wote walioshiriki katika sikukuu hiyo ni 400 ambapo 150 yatima na 250 ni wajane” amesema Annie.

Amesema lengo kubwa ni kuyafanya makundi hayo kujisikia ni sehemu ya kujumuika na wenzao ili nao wawe na furaha kama zilivyo familia nyingine.

Kwa upande wake, Tunu Pinda, mke wa waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda amewataka wajane kutokata tamaa ya maisha au kujiona wanyonge pale wanapoondokewa na wenza wao.

“Leo nimejifunza jambo kubwa sana hapa kanisani, kanisa limeonesha upendo wa hali ya juu sana kwa kuweza kukusanya idadi ya watu 400 na kula nao chakula.

“Natamani hata mimi kufanya jambo kama hili kwani ni upendo wa aina yake, napenda kusema hili nitukio kubwa na la kuigwa na watu wote,” amesema.

“Pamoja na kanisa kuhubiri neno la Mungu pia wameweza kuwajali watu kimwili kwa kushiriki nao chakula pamoja na mahitaji mbalimbali na kuwafanya kufarijika badala ya kukaa kinyonge,” amesema Tunu.

Naye Mdala Yulia ambaye ni miongoni mwa wajane walioshiriki chakula cha pamoja kanisani hapo amelishukuru kanisa kwa upendo ambao wameuonesha.

“Napenda kulishukuru kanisa kwa kuwa na maono ya kutujari sisi wajane na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na zaidi ni pale ambapo wanatuwezesha kupata mahitaji.

“Pamoja na hayo wamekuwa wakiwasaidia watoto wetu katika kuwawezesha vifaa vya shule jambo ambalo linatutia moyo kwani tunajengwa Kiroho, kimwili na kiakili kwa maana ya elimu,” amesema mdala Yulia.

error: Content is protected !!