VIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19 nchini, vinadaiwa kuingia mitini na fedha za mikopo kiasi cha Sh. 2.6 bilioni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Hayo yamebainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, akiwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, leo Alhamisi, jijini Dodoma.
“Katika ukaguzi wangu, nilishindwa kuthibitisha uwepo wa vikundi 851 katika halmashauri 19 vilivyopokea mikopo ya bilioni 2.6,” amesema CAG Kichere.
CAG Kichere amesema katika ukaguzi wake alioufanya kwenye mifuko miwili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, umebaini dosari ambapo mfuko unaosimamiwa na Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI imebainika halmashauri 46 zinadai mikopo yenye thamani ya Sh. 5.7 bilioni kutoka kwa vikundi 1,334 vilivyoacha kujihusisha na shughuli za kiuchumi.
Kuhusu mfuko unaosimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, CAG Kichere amesema wamebaini kati ya 2004 hadi 2017 ulitoa mikopo kiasi cha Sh. 475.4 milioni ambayo haijarejeshwa huku mikopo yenye thamani ya Sh. 664 milioni ikitolewa bila bima.
Leave a comment