MKUU wa Majeshi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amewasamehe vijana 853 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliofukuzwa makambini April 12, 2021 kutokana na utovu wa nidhamu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Habari, Luteni Kanali Gervas Ilonda katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika leo tarehe 5 Machi, 2022 kilichofanyika makao makuu ya jeshi, Upanga jijini Dar es Salaam.
Amesema JWTZ ina taarifa kijana mmoja kati ya wale vijana 854 waliofukuzwa amefariki na walio hai ni 853, imeamriwa vijana wote 853 warudi makambini.
Uamuzi wa kuondolewa makambini kwa vijana hao, ulitangazwa April 17, 2021 na Jenerali Mabeyo katika hafla ya kutunukiwa kamisheni kwa maafisa wapya 393 wa JWTZ na nchi rafiki.
Vijana hao walisimamishwa baada kukiuka taratibu za kijeshi kwa kuanzisha mgomo na kufanya maandamano kwenda ikulu kwa madai ya kutaka kumuona aliyekuwa rais wa wakati huo, Hayati Dk. John Pombe Magufuli.
Vijana hao walikusudia kwenda kudai kuajiriwa jeshini kama walivyoahidiwa na Hayati Magufuli, baada ya kushiriki katika ujenzi wa ofisi ya ikulu, Chamwino jijini Dodoma.
Aidha, taarifa ya kusimamishwa kwao ilieleza kwamba vijana hao walipotakiwa kusitisha mgomo huo, hawakusikia na kuendelea na mgomo wao na kuandamana, kosa ambalo jeshini linahesabika kuwa uasi.
Vijana hao ni kati ya vijana 2400 walioahidiwa kuandikishwa jeshini na walifanya uamuzi huo baada ya jeshi kuamua kuwapunguza katika kazi ya ujenzi wa Ikulu Chamwino baada ya kazi kupungua ili waende kufanya kazi katika maeneo mengine lakini wao wakapinga kwa madai wangekosa kuandikishwa jeshini.
Leave a comment