September 23, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ushahidi wa RPC Kingai alioutoa kesi ya Mbowe

Kamanda wa Polisi wa Kinondoni (RPC), Ramadhan Kingai

Spread the love

 

KAMANDA wa Polisi wa Kinondoni (RPC), Ramadhan Kingai ambaye ni shahidi namba 2 upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili kiongozi wa chaa kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu anatoa ushihidi wake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mbali na Mbowe wengine; ni Halfani Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Lingwenya.

RPC Kingai, anatoa ushahidi huo leo Jumatano, tarehe 15 Septemba 2021, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iliyopo Mawasiliano, Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake, RPC Kingai amedai shahidi namba moja Luteni Denis Urio, aliombwa na Freeman Mbowe kumtafutia wanajeshi wastaafu ili kufanya vitendo vya ugaidi, katika miji ya Moshi, Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya. Ukataji miti wa kuzuia magari, ulipangwa kufanyika kutoka Morogoro kuelekea Iringa.

Amedai, Luteni Denis Urio aliahidiwa kupewa cheo kikubwa jeshini baada ya uchaguzi mkuu kwa kuwa Mbowe atashika madaraka ya nchi.

Shahidi huyo anaeleza Mahakama kuwa watu aliowatafuta tayari wako Moshi kwa ajili ya kumdhuru Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai.

Aidha, anadai kundi hilo lilikuwa limejipanga kufanya vitendo vya kuchoma vituo vya mafuta kwa kuvilipua na masoko yenye watu wengi ili kuonesha nchi haitawaliki.

RPC Kingai anadai baada ya kuelezwa hayo, aliwasiliana na DCI, Robert Boaz na alielekeza kuundwa kwa timu ya Polisi ya kufuatilia mienendo yao kabla ya madhara kufanyika.

Anadai Adam Hassani Kasekwa, alipopekuliwa baada ya kukamatwa alikuwa na silaha aina ya luga yenye namba A 5340 ikiwa na risasi tatu ndani ya magazine. Alikutwa na kete 58 za dawa za kulevya.

Shahidi huyo anadai wakati tumewakamata, tumewaweka chini ya ulinzi nilimuelekeza ACP Jumanne awapekue maungoni.

Anadai Mohammed Lingwenya alikuwa na kete 25 za dawa za kulevya.

RPC Kingai anaendelea kutoa ushahidi wake…

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali.

error: Content is protected !!