January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ujumbe wa Askofu Bagonza kumpata Spika wa Bunge Tanzania

Dk. Benson Bagonza

Spread the love

 

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera ametoa ujumbe wenye tahadhari wa kumpata spika mpya wa Bunge la nchi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Ametoa ujumbe huo wakati chama tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimefungua dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu kuwania nafasi hiyo kuanzia tarehe 10-15 Januari 2022.

CCM kinatafuta mrithi wa Job Ndugai ambaye tarehe 6 Januari 2022, alitangaza kujizulu baada ya shinikizo kutoka kwa wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa mikoa, wabunge na makada, kutokana na kauli yake kwamba nchi itapigwa mnada kutokana na madeni.

Ndugai alitoa kauli hiyo, wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Mikaleli ya Wanyausi wa Kabila la Wagogo, mkoani Dodoma, mwishoni mwa mwaka jana ambapo alikosoa utaratibu unaoendelea wa Serikali kukopa, ni mzigo usio na tija na kuitaka Serikali iachane na mikopo ya kimataifa, kwa kuwa nchi inaweza kupigwa mnada.

Hadi jana Jumanne jioni tarehe 11 Januari 2022, wanachama wakiwemo viongozi ndani ya Bunge wamejitosa kuchukua fomu.

Askofu ametua ukurasa wake wa facebook kuzungumzia kinachoendelea picha Joseph Msukuma, Mbunge wa Geita vijijini pamoja na kuambatanisha na ujumbe wake.

Ujumbe huo wa Askofu Bagonza alioupa kichwa cha habari ‘Spika na Rais’ huu;

Chini ya Katiba yetu, katika mazingira yasiyo ya kawaida, Spika wa Bunge anaweza kuwa Kaimu Rais wetu.

Kama inakubalika kuwa katiba yetu imempa Rais madaraka makubwa, ni muhimu kuangalia pia wale wote wanaoweza kukaimu nafasi hii na kukabidhiwa madaraka hayo makubwa endapo mazingira yasiyo ya kawaida yatajitokeza.

Tabia moja ya madaraka makubwa kwa mtu ni kuwa asipoyaua madaraka, yenyewe yanaweza kumuua. Msiba mkubwa ni pale vyote viwili (madaraka makubwa na mtu) vinapoungana kuua nchi.

Mwaka 2005, CCM ilipobakiza wagombea 3 mbele ya mkutano Mkuu kabla ya kupiga kura kumchagua mmoja (JK, Mwandosya na Salim); Prof. Mwandosya alisema maneno fulani sijayasahau.

Alisema tunateua mtu atakayekuwa Rais. Na mtu huyu ndiye anayeweza kusema nchi iende vitani ikaenda, anayeweza kusema fulani anyongwe, akanyongwa. Akawataka wanachama wafanye uamuzi wa busara.

Mhimili wa Bunge ni tumaini la ustawi wa nchi. Ndilo kimbilio la wananchi. Serikali daima imeshika rungu kukusanya kodi na kulazimisha utii bila sheria.

Ni bunge tu lenye jukumu na uwezo wa kuiambia serikali telemsha rungu lako, shika adabu yako, tafakari kabla ya kutenda.

Uwezo wa Spika na busara zake nje ya vigezo vya kiitikadi ni muhimu sana. Tuache utani katika mambo muhimu ya nchi.

Spika anaweza kutakiwa kufanya maamuzi mazito kuhusu nchi na kwa hiyo afya ya akili, ya mwili, ujuzi na uzoefu wake kimataifa visitiliwe shaka.

Waliokwisha kuchukua fomu ni, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson na Mwenyekiti wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu.

Wabunge waliokwisha kujitokeza kuchukua fomu ni pamoja na Godwin Kunambi wa Mlimba, Emmanuel Mwakasaka wa Tabora Mjini na Joseph Kasheku ‘Msukuma’ wa Geita Vijijini.

Wengine ni, Dk Saimon Ngatunga, Tumsifu Mwansamale, Melkion Ndofu, Ambwene Kajula, Patrick Nkandi na Hamidu Chamani.

Waliowahi kuwa wabunge na mawaziri katika serikali ya awamu ya nne ni, Sophia Simba ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa Chama Cha mapinduzi (UWT) pamoka na Stephen Masele.

Masele akiwa mbunge wa Shinyanga Mjini, alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa Bunge la Afrika (PAP).

Wengine ni, Goodluck Ole-Madeve, Juma Chuma, Baraka Byabato na msomi mwenye shahada mbalimbali tisa, Profesa Handley Mafwenga.

error: Content is protected !!