May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Barabara ya Chamwino kufungwa ‘smart camera’

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka

Spread the love

 

KATIKA kudhibiti ajali za mara kwa mara sambamba na watoto kugongwa katika barabara Kuu ya Dodoma – Dar es Salaam eneo la Buigiri Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, serikali imepanga kufunga kamera za kisasa ‘smart camera’ kwa lengo la kunasa magari yanayopita kwa kasi katika eneo hilo. Anaripoti Danson Kaijage – Dodoma… (endelea)

Hayo yameelezwa na Diwani wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka wakati akifungua madarasa yaliyojengwa kwa mradi wa fedha za COVID-19 katika shule ya Sekondari wa Buigiri.

Yindi amesema kata hiyo ina shule sita na barabara Kuu imepita katika vijiji vitatu.

“Wanafunzi wengi wanagongwa na magari yanayopita kwa kasi eneo hilo bila kuzingatia usalama. Wanafunzi na hata wananchi wanapoteza maisha kutokana na ajali hizi za mara kwa mara,” amesema.

Yindi amesema alitembelea maeneo mbalimbali nchini yaliyopitiwa na barabara kuu ili kuona namna gani wataweza kuepukana na ajali na kwenye baadhi ya barabara kuu.

“Tumeshafanya kikao na kamanda wa kikosi cha usalama barabarani na kupeleka ombi rasmi kwa kutumia wataalam wa ICT tutafunga kamera nne’ amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema suala la kufungwa kamera ni zuri.

“Fungeni hizo kamera huenda tukapata suluhisho la ajali,” amesema.

Alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Gift Msuya na vyombo vya ulinzi na usalama waone jinsi gani jambo hilo litafanyika.

Awali akipokea taarifa ya ujenzi wa madarasa hayo ilielezwa kuwa Buigiri Sekondari ilipokea jumla ya Sh milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu na Ofisi ya Walimu Ofisa elimu Mkoa wa Dodoma.

Alisema ujenzi wa madarasa umekamilika na ifikapo tarehe 17 Januari, 2022 watoto wote watakuwa wameripoti shuleni.

Amesema watafanya kampeni kuhakikisha watoto wanaripoti shuleni bila kuwa na visingizio vya kukosa sare na daftari na mahitaji mengine ili kazi ya kufundisha uanze mara moja kwa wanafunzi wote.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbanga alisems chama hicho kinawashukuru wote waliohakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati.

Amesema wilaya ya Chamwino imepata fedha kiasi cha Sh bilioni 2.92, fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 146, shule shikizi 64 huku shule za sekondari zikiwa nane.

error: Content is protected !!