January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu kizimbani kwa madai ya kumbusu, kumnyanyasa kingono muumini

Spread the love

 

Askofu mmoja anayehusishwa na kanisa la Kianglikana jijini Nairobi nchini Kenya, ameshtakiwa kwa kumnyanyasa mwanamke mmoja kwa kumshika matiti na kujaribu kumbusu bila idhini yake. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Askofu Joel Waweru alishtakiwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Kibera, Derrick Kuto na kukanusha makosa mawili yanayohusiana na unyanyasaji wa kingono ambayo yanamkabili.

Kwa mujibu wa jalada la mashtaka, kasisi huyo alitenda kosa hilo tarehe tofauti na nyakati tofauti katika kaunti ndogo ya Lang’ata, kaunti ya Nairobi.

Karatasi ya mashtaka iliyosomwa kortini ilisema kwamba Waweru akiwa mtu mwenye mamlaka aliendelea kumtongoza mwanamke aliyefahamika kwa ufupisho wa jina la J.N.M huku akijua kuwa mwanamke huyo alimkataa.

Mshukiwa alishtakiwa kwa kosa la pili la kushika titi la J.N.M kwa njia isiyofaa tarehe 13 Julai, 2021.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi iliyowasilishwa mahakamani hapo, mshtakiwa anadaiwa kumnyanyasa mwanamke huyo kingono tangu 2018.

Mahakama iliarifiwa kwamba mwanamke huyo ambaye pia alikuwa mmoja wa viongozi wa kanisa hilo, alishushwa cheo na baadaye akahamishwa na kupelekwa katika kanisa tofauti huku mshahara wake ukikatwa.

Ripoti hiyo ya polisi ilisema mwanamke huyo alilalamika kwamba askofu huyo kwa nyakati tofauti alimwaibisha na kumtaka awaambie waumini kwamba hajawahi kumwagiza washiriki ngono baada ya uvumi kuanza kuvuja.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, mwanamke huyo pia aliwaambia polisi kwamba askofu huyo pia alijaribu kumbusu lakini mkewe aliingia ofisini na hakuona chochote.

Ripoti ya polisi inaeleza zaidi kuwa siku moja akiwa na doa kwenye blauzi yake, mtumishi wa Mungu alifika ofisini mwake na kumshika matiti mahali doa lilipokuwa kwa njia isiyofaa, jambo ambalo lilimfanya akose raha na utulivu.

Aliripoti kwa polisi kwamba askofu huyo aliendelea kumwambia kwamba yeye ni mrembo na anampenda.

Ripoti ya polisi inasema kuwa, mwanamke huyo anahisi Askofu ana hisia za kimapenzi kwake ilhali akitambua kuwa ameolewa.

Polisi wanasema kwamba mwanamke huyo alihisi aibu na kuchanganyikiwa kihisia na kuhisi kutokuwa salama.

Hata hivyo, askofu huyo alikana mashtaka hayo yote na kuomba apewe masharti nafuu ya dhamana.

Kuto alimwachilia kwa dhamana ya Shilingi za Kenya 50,000 (sawa na T SH milioni moja) pesa taslimu na kuahirisha kesi hiyo hadi itakapotajwa tena baada ya wiki mbili.

error: Content is protected !!