August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TRA wazua kizaazaa Mwanza

Wananchi wa Jiji la Mwanza wakiwa wamepanga foleni nje ya Jengo la Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania Kanda ya Mwanza

Spread the love

SHUGHULI za kijamii na kiuchumi zimesimama jijini Mwanza, kwa zaidi ya saa sita kutokana na baadhi ya barabara za katikati ya Jiji kufungwa na wananchi waliokuwa wamepanga foleni kwenda kulipa kodi ya majengo leo tarehe 30 Juni, 2017, anaandika Moses Mseti.

Ilikuwa majira ya saa kumi na moja alfajiri ambapo msongamano wa watu ulianzia katika barabara ya Kinyata hadi ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zilizopo barabara ya Kamanga feri.

Wananchi hao wamesema kuwa wameamka saa kumi alfajiri lakini utoaji wa huduma katika ofisi hizo unasuasua na kusababisha msongamano mkubwa wa watu ingawa walikuwa walikuwa wakifika ofisi za TRA siku za nyuma lakini mitambo yao ilikuwa ikiharibika mara kwa mara.

“Tunaomba muda wa kulipa kodi ya majengo uongezwe, tangu watangaze mwisho wa kulipa tumekuwa tukifika hapa, lakini hatukubahatika kupata huduma kutokana na wingi wa watu waliokuwepo.

“Tatizo si la wananchi, hapana. Tangu miezi miwili iliyopita tulikuwa tunakuja hapa (TRA), lakini huduma ilikuwa inasuasua, hivyo ni bora watuongezee muda kwani kosa ni la kwao,” amesema Ally Mbaraka mmoja wa wananchi waliokutana na adha hiyo.

Ernest Dundee, Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza, amesema watahakikisha wanatoa huduma hiyo hadi pale watu waliofika leo wahudumiwe na kuisha, na kwamba wapo tayari kuwahudumia mpaka saa tatu usiku.

John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, amesema baadhi ya wananchi ni wazembe katika kushughulikia suala linalohusu maisha yao ikiwemo kushindwa kulipa kwa wakati kodi ya pango ya nyumba kitendo hivi sasa kimesababisha kero.

“Hili zoezi la kulipa kulipa kodi ya pango lilikuwa ni la mwaka mzima lakini kutokana na tabia yetu sisi watanzania muda ukiisha ndio unatuona tunaanza kushughulika nayo, hata sasa hivi tukiongeza muda wengine watarudi kulala,” amesema Mongella.

Zoezi la ulipaji wa kodi ya majengo nchi nzima ambao lilianza tarehe 1 Juni, 2016 na unatarajiwa kukamilika leo tarehe 30 Juni, 2017.

error: Content is protected !!