June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yakaza masharti kukabili ugonjwa wa Korona

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imetoa mwongozo mpya wa kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa korona (UVIKO-19). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam, … (endelea).

Mwongozo huo umetolewa leo Jumapili, tarehe 25 Julai 2021 na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

“Kutokana na mwenendo wa ugonjwa wa Korona (UVIKO-19) nchini, Kamati ya Wataalamu imeainisha maeneo mahsusi yanayohitaji kutiliwa mkazo kupitia afua za kupunguza msongamano katika jamii. Lengo ni kukata mnyororo wa maambukizi katika ngazi ya kaya na jamii,” amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi ameongeza “mwongozo huu utawawezesha Wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii sambamba na kubadili tabia zao, huku wakizingatia mbinu za kujikinga na ugonjwa, kwa kupata elimu ya kutosha, na kujiwekea utaratibu wa kudhibiti ugonjwa kutokusambaa kwenye jamii.”

Prof. Makubi amesema, mwongozo huo unasitisha mikusanyiko yote mikubwa ya kijamii, kidini na kisiasa,  hadi ugonjwa huo utakapo dhibitiwa.

“Pale ambapo panahitajika ulazima wa kufanyika shughuli ya mikusanyiko, kibali kiombwe kuanzia ofisi za serikali za mitaa, kupitia halmashauri na idhini itolewa na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa husika, kwa kuzingatia vigezo vyote vya kinga na usalama wa afya kwa wananchi,” amesema Prof. Makubi.

Kwa mujibu wa muongozo huo uliotolewa na Prof. Makubi, mikusanyiko katika maeneo ya umma ikiwemo  stendi za mabasi, nyumba za ibada, vituo vya kutoa huduma za afya, baa na masoko,   imezuiwa huku uvaaji barakoa ikiwa ni takwa la lazima, kwa wananchi waliko katika maeneo hayo.

“Kila msafiri anayeingia kwenye chombo cha usafiri wa umma, lazima awe amevaa barakoa kama ilivyoelekezwa kwenye mwongozo, isipokuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka nane,” amesema Prof. Makubi.

Muongozo huo unaelekezea wananchi kupimwa UVIKO-19, katika sehemu hizo.

“lazima kupima joto mwili kwa kutumia ‘thermoscanners’ ufanyike getini na kwenye mabasi.Halmashauri zisimamie maeneo yote ya mabasi yaendayo mikoani,  yaanzishe utaratibu wa uchunguzi wa wasafiri na wale watakaoonesha dalili  wasiruhusiwe kuendelea na safari badala yake washauriwe kwenda kuonana na wahudumu wa afya,” amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi amesema, muongozo huo unaelekeza waumini katika nyumba za ibada, kukaa umbali wa mita moja kutoka mtu mmons hadi mwingine.

“Ibada ziwe za muda mfupi usiozidi masaa mawili, huduma zinazohusisha kugusana ziepukwe. Kuwepo na ujumbe wa mara kwa mara kwa ajili ya kuwakumbusha waumini kuhusu namna ya kujikinga na UVIKO-19 na namba za kuwasiliana na huduma za afya iwapo atapatikana mgonjwa,” amesema Prof. Makubi.

error: Content is protected !!