SERIKALI ya Tanzania, imeanzisha mikakati ya kumaliza changamoto za mawasiliano, katika maeneo ya pembezoni mwa nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mikakati hiyo imetajwa leo tarehe 26 Julai 2021 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile, akizindua Studio za Redio Jamii inayosimamiwa na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), jijini Dodoma.
Waziri huyo wa mawasiliano amesema, mkakati wa kwanza ni kupunguza gharama za leseni za redio zilizopo au zitakazoanzishwa katika maeneo hayo.
“Tunakwenda kupunguza gharama za leseni kwa redio zitakazokuwa ngazi ya wilaya, jamii na katika maeneo ya pembezoni. Tunataka katika maeneo yote yale ambayo wenzetu wamekuwa wanasikiliza redio nchi jirani, tuondokane nayo,” amesema Dk. Ndugulile.
Mkakati mwingine uliotajwa na Dk. Ndugulile, ni kutoa tenda za miradi ya mawasiliano ya simu, katika maeneo hayo.
“Tumetoa tenda ya mawasiliano katika mawasiliano ya simu, maeneo ambayo yako pembezoni mwa nchi. Tayari zabuni tumetangaza ili makampuni ya simu yawekeze katika usikivu wa simu kwenye maeneo hayo,” amesema Dk. Ndugulile.
Dk. Ndugulile amesema, mikakati hiyo imelenga kuwaondolea wananchi wa maeneo ya pembezoni, changamoto ya kupata mawasiliano kutoka katika vyombo vya mawasiliano vya nchi jirani.
“Lengo letu muda mfupi ujao mawasiliano yanayosikika yawe ya Tanzania, badala ya sasa maeneo ya pembezoni kumekuwa na usikivu wa mawasiliano ya nchi jirani,” amesema Dk. Ndugulile.
Leave a comment