Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Spika Ndugai: Dk. Mpango amepoteza sifa ya ubunge, NEC…
Habari za Siasa

Spika Ndugai: Dk. Mpango amepoteza sifa ya ubunge, NEC…

Spika Job Ndugai
Spread the love

 

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuwa Jimbo la Buhigwe, mkoani Kigoma liko wazi baada ya mbunge wake, Dk. Phillip Mpango, kupoteza sifa ya ubunge. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Dk. Mpango amepoteza sifa, baada ya kupendekezwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuwa Makamu wa Rais kisha kuthibitishwa na Bunge kwa asilimia 100.

Spika Ndugai ametoa taarifa hiyo leo Jumanne tarehe 30 Machi 2021, bungeni jijini Dodoma, muda mfupi baada ya Dk. Mpango kuthibitishwa na Bunge kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

Dk. Mpango alithibitishwa na Bunge kuwa Makamu wa Rais, baada ya kupata asilimia 100 ya kura zote zilizopigwa na wabunge 363, waliohudhulia kikao hicho.

Akitoa taarifa hiyo, Spika Ndugai amesema hatua hiyo ni matakwa ya Katiba ya Tanzania Ibara ya 71, inayoelekeza mambo yatakayomfanya mbunge kukoma ubunge wake.

“Nitoe taarifa ifuatayo, Katiba ya Tanznaia inatoa maelekezo kuhusu muda wa wabunge kushika madarakani, Ibara ya 71 inaorodhesha mambo ambayo kwayo mbunge atakoma kuwa mbunge, miongoni mwake ni iwapo anateuliwa kuwa makamu wa rais,” amesema Spika Ndugai

“Uthibitisho huu unamuondolea sifa Dk. Mpango kuendelea kuwa Mbunge wa Jimbo la Buhigwe, hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ninawajibika kuitaarifu NEC kwamba kiti cha ubunge cha Buhigwe sasa kiko wazi.”

Dk. Mpango aliiongoza Buhigwe katika kipindi cha miezi mitano baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2020.

Akitoa salamu zake kwa wananchi wa Buhigwe, Dk. Mpango amewashukuru kwa kumchagua katika uchaguzi huo, kuwa mbunge.

“Kwa kuzungumza na wananchi ambao wako mbali kidogo na hapa tulipo, ni ndugu zangu wananchi wa Buhigwe ambao walinichagua kwa kura asilimia 77 ili niwe muwakilishi wao hapa bungeni, kwanza naendelea kuwashukuru kwa heshima waliyonipa,” amesema Dk. Mpango.

Dk. Mpango amewaomba wabunge wa mkoa wa Kigoma kuendelea kuwawakilisha bungeni wananchi wa Buhigwe na wa mkoa huo.

Dk. Philip Mpango

“Bado Buhigwe ndio kwetu, nitaendelea kuwa karibu nao na mimi nawaombea na imani kabisa watapata muwakilishi mwingine mahiri kwa ajili ya kusemea matakwa yao na shida zao katika Bunge hili.”

“Lakini pia waheshimiwa wabunge wa Kigoma wataendelea kuwa sauti ya wananchi hao wa Buhingwe na Kigoma kwa ujumla,” amesema Dk. Mpango.

Dk. Mpango anachukua nafasi ya Mama Samia, ambaye ameapishwa kuwa Rais wa Tanzania, kufuatia kifo cha Hayati Dk. John Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam.

Dk. Mpango ataapishwa kesho Jumatano, tarehe 31 Machi 2021, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!