May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mpango kuendeleza miradi ya Magufuli

Spread the love

 

MAKAMU wa Rais mteule wa Tanzania, Dk. Phillip Mpango, ameahidi kuiendeleza miradi ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, ili kuwafuta machozi Watanzania kufuatia kifo chake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … endelea).

Hayati Magufuli, alifikwa na mauti akiwa madarakani Jumatano ya tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na mwili wake kuzikwa nyumbani kwao, Chato mkoani Geita.

Miongoni mwa miradi hiyo ni, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere maarufu Stigler’s Gorge, miundombinu ya barabara na madaraja.

Dk. Mpango ametoa ahadi hiyo leo Jumanne tarehe 30 Machi 2021, bungeni jijini Dodoma, baada ya kuthibitishwa na mhimili huo kuwa Makamu wa Rais, baada ya kupendekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Jinsi ambavyo bodaboda waliamua kuchukua kazi ya polisi barabarani kumsindikiza Dk. Magufuli ni ishara wazi ya wanyonge kutuambia kazi zote alizoacha kiongozi wetu zisipokwenda vizuri hatuna namna, sijui kama mliwasikia walivyokuwa wanaimba,” amesema Dk. Mpango.

Dk. Mpango amesema”kwa hiyo wajibu wa kuhakikisha kwamba ndoto za wanyonge hawa Watanzania wanataka miradi, wanataka SGR yao ikamilike, wanataka Bwawa la Mwalimu Nyerere likamilike, wanataka mabarabara na hususan za vijijini zikamilike, wanataka huduma za afya ziwe bora zaidi, wanataka maji, wanataka usalama waendelee kufanya shughuli zao.”

Dk. Philip Mpango

Dk. Mpango atakayeapishwa kesho Jumatano Ikulu ya Chamwoni mkoani Dodoma amesema, Watanzania wanataka kuona mambo yaliyoasisiwa na Dk. Magufuli yanafanyiwa kazi, ili kuwaletea maendeleo.

“Watanzania hawataki rushwa, nachotaka kusema ni nini, nataka kusema kama bunge la Tanzania litanihitibitisha katika nafasi niliyopendekezwa na rais, haya ndiyo mambo nitakayokwenda kumsaidia ili nchi yetu isonge mbele, wananchi hawa kiu yao ya maendeleo iweze kutimia,” ameahidi Dk. Mpango.

Mwanasiasa huyo amesema atahakikisha anamsaidia Rais Samia kuikamilisha miradi hiyo, ili kuenzi mchango wa Dk. Magufuli.

error: Content is protected !!