SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewataka wabunge wanne wa ACT-Wazalendo, kwenda bungeni kuapishwa ili waanze kuwatumikia wananchi waliowachagua. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo Ijumaa tarehe 11 Desemba 2020 muda mfupi baada ya kumaliza kumwapisha Profesa Shukrani Manya kuwa Mbunge wa kuteuliwa.
Profesa Manya, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, ameteuliwa kuwa mbunge na Rais John Pombe Magufuli ambaye pia, amemteua kuwa Naibu Waziri wa Madini.
Mara baada ya kumaliza kumwapisha, Spika Ndugai amesema, Bunge hilo halitaki kurudisha nyuma kasi ya Serikali na amekuwa akiwaapisha wabunge pindi wanapoteuliwa.
Spika Ndugai amesema, wabunge wanne wa ACT-Wazalendo ambao bado hawajaapa kama wana nia ya kuitumikie nchi yao “kama kweli waliomba ubunge kuwatumikia wananchi, hawana sababu ya kuendelea kuzulula huko waliko, watoe taarifa haraka kwa spika, tuwapangie ili wapate kiapo waendelee kufanya kazi za kibunge kama wananchi walivyowaamini. Nadhani ni watatu.”

Hatibu Said Haji (Konde), Salum Mhamed Shafi (Chonga), Omar Ali Omar (Wete) na Khalifa Mhamed Issa wa Mtambwe wote kutoka Pemba visiwani Zanizbar
Mara baada ya kauli hiyo, MwanaHALISI Online limezungumza na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema, wao kama chama tayari wamekwisha kutoa msimamo wa kuwaruhusu madiwani, wawakilishi na wabunge kwenda katika vyombo vya uwakilishi.
“Tunawaruhusu wabunge wote kwenda bungeni na ACT-Wazalendo hakuna tena zuio kwenda katika vyombo vya uwakilishi. Iwe diwani, mbunge na wawakilishi. Hivyo, watakwenda tu hakuna tatizo,” amesema Shaibu.
Leave a comment