Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa THDRC yakumbusha machungu uchaguzi mkuu, yasisitiza mazungumzo
Habari za Siasa

THDRC yakumbusha machungu uchaguzi mkuu, yasisitiza mazungumzo

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Kituo cha Watetezi wa Haki za Binadamu Taifa
Spread the love

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umeishauri Serikali nchini humo kufanya mazungumzo na vyama vya upinzani ili kupata suluhu ya changamoto zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limetolewa jana Alhamisi tarehe 10 Desemba 2020 na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, wakati anatoa hotuba yake kuhusu maadhimisho ya siku ya haki za binadamu duniani.

“Sisi tuna amini, mazungumzo ndio chanzo cha kuleta haki na huondoa ukiukwaji wa haki za binadamu na ndio mwanzo wa kutibu majeraha yaliojitokeza katika uchaguzi uliopita,” alisema Olengurumwa.

Vyama vya upinzani ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi viligoma kutambua matokeo ya uchaguzi huo yaliyokipa ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi wa Urais wa Tanzania na Zanzibar, ubunge, uwakilishi na udiwani.

Vyama hivyo vilipinga matokeo hayo kwa madai mchakato wake haukuwa huru na wa haki na kutoa wito kwa Serikali kuitisha meza ya majadiliano kwa ajili ya kutafuta suluhu ya malalamiko yao.

Akiziungumzia malalamiko hayo, Olengurumwa alisema njia sahihi ya kutibu majeraha ni meza ya majadiliano.

“Tunafahamu uchaguzi uliopita ulikuwa na changamoto, kuna watu walioumia na wengine kupoteza maisha, wengine wamepoteza haki zao za kisiasa, lakini haya yote yatatatuliwa endapo Taifa litajenga utamaduni wa kukaa, kuelezana ukweli na kukubaliana kutorudia makosa,” alisema Olengurumwa.

Rais John Magufuli

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli alishinda urasi wa Tanzania kwa asilimia 84 ya kura zilizopigwa milioni 15.

Huku Dk. Hussein Mwinyi aliyegombea urais wa Zanzibar, alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 76.27. Katika uchaguzi huo, CCM ilizoa viti vingi vya ubunge wa majimbo na viti maalumu huku Chadema kikiambulia jimbo moja na viti maalumu 19.

Wakati na CUF kikiambulia jimbo moja Bara na ACT-Wazalendo kikipata majimbo manne Zanzibar.

Maalim Seif Sharrif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Hata hivyo, ACT-Wazalendo kimefanya maridhiano na Serikali ya Zanzibar kwa kukubali kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa kumpendekeza Maalim Seif Shariff Hamad, aliyekuwa mpinzani wa Rais Mwinyi kwenye uchaguzi huo, kuwa makamu wa kwanza wa rais.

Olengurumwa amepongeza uamuzi huo wa ACT-Wazalendo kukubali maridhiano na Serikali ya Zanzibar, na kushauri jitihada hizo zifanyike kwa upande wa Bara.

“Tunaamini kilichofanyika Zanzibar huenda ndio mwanzo wa kuondoa changamoto ambazo zingeweza kujitokeza katika chaguzi zijazo na kwa upande wa Bara, kumekuwa na sintofahamu baina ya vyama kama Chadema na  CCM,” alisema.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

Olengurumwa alisema “nawaomba waone umuhimu wa kukutana, kujadiliana na kutatua changamoto zilizojitokeza na kuweka muafaka wa kuzuia kutokea kwa changamoto kama hizo katika chaguzi zijazo.”

Olengurumwa amesema, Tanzania inapaswa kutatua matatizo yake yenyewe badala ya kusubiri waamuzi kutoka nje.

“Wakati mwingi amani imekuwa ikipotea au ikichezewa wakati wa chaguzi au baada ya chaguzi hivyo tunaamini ushauri tunaoutoa ukifanyiwa kazi manug’uniko na ukiukwaji wa haki za binadamu uliojitokeza katika uchaguzi unaweza ukapatiwa muafaka katika meza ya mazungumzo.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti Chadema Taifa

“Na baadae nchi yetu ikawa imetibu changamoto hizi kuelekea katika chaguzi zingine zijazo,” alisema Olengurumwa.

Akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu Dunini, Olengurumwa ameiomba Serikali kuboresha ulinzi na mazingira ya utendaji kazi wa watetezi wa haki za binadamu nchini.

1 Comment

  • Ni jambo muhimu sana kwa nchi yetu viongozi wa kambi zote kukutana pamoja na kuchukua hatua mapema kufanya maridhiano ili mbele twendako kusitokee malalamiko wakati wa chaguzi. Mafanikio ya Zanzibar iwe mfano na Bara/Tanganyika waige….watu wataipenda nchi yao na kuepusha wimbi la wakimbizi na watu wenye ujuzi kuhama. inaonesha wazi matokeo kwa baadhi ya majimbo ni mshangao wa wengi. upinzani mzuri ukiwepo unasaidia kasi ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari za SiasaTangulizi

CAG aibua madudu halmashauri 10, TANESCO na MSD

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!