Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Siri za Serikali ya JPM na Acacia zafichuka 
Habari za SiasaTangulizi

Siri za Serikali ya JPM na Acacia zafichuka 

Rais John Magufuli alipokutana na viongozi wa Acacia
Spread the love

KAMPUNI ya madini ya ACACIA Mining (PLC), imeuzwa rasmi kwa kampuni ya Barrick Gold Corporation zote kutoka nchini Canada. Mauzo hayo yamefanyika, huku serikali ya Tanzania, “ikiangukia pua kweye madai yake.” Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Katika taarifa yake kwa umma, Barrick Gold Corpation inasema, imenunua hisa zote za kampuni ya ACACIA kwa thamani ya dola za Marekani 428 milioni (Sh. 2.2 trilioni).

Makubaliano haya yanafungwa baada ya kumalizika mvutano uliodumu kwa takribani miezi mitano kuhusu thamani halisi ya kampuni ya Acacia.

Machi mwaka 2017, ACACIA iliingia kwenye mvutano na serikali kuhusiana na mchanga wa dhahabu unaosafirishwa nje ya nchi na kampuni hiyo.

Taarifa zinasema, kabla ya kuibuka kwa sakata la makanikia, kampuni ya Acacia ilikuwa na thamani ya dola za Marekani 4,400 milioni (takribani Sh. 10 trilioni).

Kwa mujibu wa kanuni za Masoko ya Hisa na Mitaji, taarifa za manunuzi ya makampuni huwekwa wazi pamoja na nyaraka nyengine zinazohusika.

Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na Mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, kupitia mauziano hayo, nyaraka zote muhimu ambazo serikali ya Rais John Magufuli ilizifanya kuwa siri, zimeanikwa kupitia makubaliano hayo ya mauzo.

Miongoni mwa nyaraka zilizoanishwa, ni pamoja na makubaliano kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya Barrick yaliyohusu kumalizika kwa mgogoro wa makanikia na masuala ya kodi.

Nyaraka hiyo ambayo ilifanywa kuwa siri kuu na Prof. Palamagamba Kabudi, aliyekuwa waziri wa katiba na sheria wakati huo na kiongozi wa  timu ya majadiliano ya serikali, imewekwa kama kiambatanisho namba 4 cha nyaraka za manunuzi ya Acacia.

Kwa mujibu wa Zitto, nyaraka hizo zinaonyesha kuwa Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na Barrick Gold Corporation mnamo tarehe 19 Mei 2019.

Zitto anasema, “makubaliano hayo ni mabaya, ya hovyo, yasiyo ya kizalendo na yanayoumiza nchi kuliko makubaliano yaliyokuwepo kwa mujibu wa sheria ya Madini ya mwaka 2010.”

Anaongeza, “kwa ufupi tu ni kuwa Rais John Pombe Joseph Magufuli na Waziri Palamagamba Kabudi wameuza nchi kwa vipande vya dhahabu. Kiambatanisho Na. 4 kimeweka muhtasari wa kinachoitwa ‘Material Terms’ katika makubaliano ya awali kati ya Serikali na Barrick Gold ambayo yamesainiwa (INITIALED)  Mei mwaka huu.

Zitto ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Tume ya Rais ya Madini ambayo iliongozwa na aliyepata kuwa mwanasheria mkuu wa kwanza wa Tanganyika, Jaji Mark Bomani anasema, “ni masikitiko makubwa kuwa serikali yetu haijathubutu hata kuliambia Bunge kuhusu kuwapo kwa makubaliano na kampuni hiyo.”

Kampuni ya Barrick imelazimika kuweka taarifa hizo, kufuatia matakwa ya kanuni za masoko ya mitaji yanayoelekeza kuweka wazi makubaliano hayo.

“Makubaliano haya yamesainiwa wakati Bunge likiwa linaendelea na mkutano wake jijini Dodoma. Sisi kama wawakilishi wa wananchi imebidi kusubiri  masoko ya mitaji ya ‘Mabeberu’ wa London yaweke wazi masuala yanayohusu nchi yetu. Hii ni dharau kubwa ambayo Serikali ya Rais Magufuli imefanya kwa wananchi na kwa Bunge,” ameeleza.

Kwa mujibu wa taarifa ya Zitto ambayo anasema ameipata kutoka kwenye soko la mitaji la London, serikali imekubaliana na Barrick kulipwa kiasi cha dola za Marekani 300 milioni (Sh. 700 bilioni), kama malipo ya kumaliza mgogoro wote (full, final and complete settlement) na siyo kishika uchumba kama ilivyoeleza umma.

Kampuni ya Barrick italipa kiasi hicho cha fedha kwa muda wa miaka saba na zitatolewa baada ya kuondoa madai yote ya kodi ambayo Acacia inaidai serikali ya Tanzania.

Acacia Group ina madai ya marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT Refunds), yanayofikia takribani dola za Marekani 240 milioni (Sh. 552 bilioni).

Hivyo katika malipo hayo ya dola za Marekani 300 milioni, kuna uwezekano mkubwa wa fedha itakayobaki baada ya kutoa VAT kuwa dola 60 milioni (Sh.138 Bilioni) tu.

Aidha, kampuni ya Barrick Gold wamesamehewa kodi ya ongezeko la mtaji la dola za Marekani 85.6 milioni, katika makubaliano hayo. Mbali na msamaha wa ongezeko la mtaji, serikali imetoa msamaha kwa kampuni hiyo kwa kodi ya  ‘Capital Gains’ ambayo inatokana na mauzo ya hisa za Acacia kwa Barrick.

Mwaka 2012, Bunge lilitunga sheria ya kutoza kodi ya ongezeko la mtaji kwa mauzo ya mali zilizopo nchini ili kudhibiti ukwepaji wa kodi.

Zitto anasema, “Barrick inainunua Acacia kwa hisa ambazo Barrick haikuwa inamiliki ambazo zimepewa thamani ya dola 428 milioni. Capital Gains Tax ya 20 asilimia ilipaswa kulipwa. Lakini Rais Magufuli na Prof. Kabudi wametoa msamaha na kuipoteza serikali mapato yake halali na ya kisheria ya dola 85.6 milioni (karibu Sh. TZS 200 bilioni).

“Tukirejea hoja ya kwanza hapo juu utaona kuwa sio tu Tanzania kiuhalisia haitapata Dola Milioni 300, bali pia tunaipa zawadi Barrick ya dola Milioni 25.6 (zaidi ya Sh. 59 Bilioni) za ziada.”

Zitto anakiri kuwa serikali imeahidiwa kupewa asilimia 16 ya hisa kwenye Barrick. Hata hivyo, anadai kuwa hisa hizo ni daraja B na wamekubali kupoteza umiliki wa asilimia 30 kupitia soko la hisa la Dar es Salaam (DSE).

Anasema, “ni kweli serikali itapewa hisa za bure 16 asilimia kwenye kampuni tanzu zote za Acacia hapa nchini kama tulivyoambiwa na Serikali yenyewe. Lakini hisa hizo ni za daraja la B ambazo ni hisa dhaifu kulinganisha na zile za daraja la kwanza.

“Hisa za aina hii, haziruhusiwi kuuzwa, hazina kura kwa masuala fulani fulani ya kampuni na huwezi hata kuziweka kama dhamana ya mikopo. Hata mgawo wa gawio, hisa hizi hupata baada ya wale wa daraja A kulipwa kwa ukamilifu.”

Anasema, “licha ya makubaliano haya ya hovyo na yasiyo na tija, serikali yetu imetoa msamaha kwa Barrick kutoorodhesha hisa zake kwenye soko la hisa nchini.”

Anasema, sheria ya madini ya mwaka 2010, ambayo ilitungwa wakati William Ngeleja, akiwa waziri wa nishati na madini, iliweka sharti kwamba ni lazima makampuni ya madini yauze asilimia 30 ya hisa zake kwa Watanzania kupitia soko lao la hisa.

“Makubaliano ya Mei 2019 kati ya Barrick na Serikali yametoa msamaha kwa Barrick kutotekeleza sharti hilo la kisheria. Uamuzi huu unavunja sheria za nchi, ni hujuma kwa Watanzania kumiliki maliasili zao na ni ukosefu wa maarifa ya kiuchumi kwa kiwango kisichomithilika wala kuvumilika,” anaeleza Zitto kwa lugha ya kukasirika.

Anasema, Serikali na Barrick, wamekubaliana pia kuwa baada ya mkataba wao kukamilika, Bunge la Tanzania haliwezi kutunga sheria yeyote ambayo itabadili makubaliano hayo na kodi zote zilizokuwa zinafanya kazi wakati wa kuingia makubaliano hazitaweza kubadilishwa kipindi chote ambacho Barrick watakuwa wanafanya kazi nchini (fiscal stabilisation).

Anasema, “makubaliano ya namna hii ndiyo kitu kilicholeta Buzwagi mwaka 2007 ambapo Serikali za Rais Benjamin Mkapa na Rais Jakaya Kikwete ziliingia mikataba ya kulifunga Bunge kutimiza majukumu yake ya kikatiba kama dola (sovereign).

“Sheria ya Madini ya mwaka 2010, iliondoa sharti hili kufuatia mapendekezo ya Kamati ya Bomani. Rais Magufuli na Waziri Kabudi wameturudisha kwenye unyonyaji ule ule ambao tulishaukataa.”

Kuhusu masuala ya kisheria, kampuni ya Barrick imeruhusiwa – pale kutakapotokea mgogoro wa kisheria na serikali ya Tanzania – kufungua  shauri la madai kwenye mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara, kinyume na sheria mpya za madini ya mwaka 2017. Sheria inataka makampuni yote ya madini, kutofungua mashauri yake nje ya Tanzania.

“Migogoro yote inapaswa kushughulikiwa na mahakama za ndani ya nchi. Serikali ya Tanzania imekubaliana na Barrick kuwa migogoro itafanyika kwa mujibu wa kanuni za UNICITRAL na Rais wa Kituo cha usuluhishi wa migogoro cha Singapore ndio atateua wasuluhishi ambao hapatakuwa na Mtanzania.

“Serikali mara zote iliambiwa kuwa mabadiliko ya sheria kuhusu ‘arbitration’ hayakuwa halisi na ni ulaghai. Serikali yenyewe imekuwa ya kwanza kuvunja sheria yake yenyewe kwa kuingia makubaliano na Barrick Gold kuwa Mahakama zetu hazitahusika na kutatua mgogoro wowote kati ya Barrick na Tanzania,” anafafanua.

Anaongeza: “Siku za mwanzo kabisa za mgogoro wa Makanikia nilieleza kuwa Serikali ya Rais Magufuli haina maarifa ya kuwezesha nchi kupata ushindi katika suala hili, watu wengi walinitukana, lakini leo imedhihirika hivyo.

“Wakati ule nilitoa mfano kuwa Acacia ilipotaka kununuliwa na kampuni nyengine ya Canada kwa thamani ya dola za Marekani 4.4 bilioni (Sh. 10 trilioni). Tanzania ingefaidika sana kwa kupata kodi ya ongezeko la mtaji ya dola za Marekani 880 milioni (Sh. 2 trilioni). Serikali haikufanya subira na ikazuia Makanikia na mpango ule wa Acacia kununuliwa ukavunjika.

“Leo Serikali yetu imekwenda kuingia makubaliano ya aibu kabisa ambayo kiuhalisia tunaishia kufuta kesi za Kodi ya Dola za Marekani 190 Bilioni (Sh. 400 trilioni) na tunawalipa Barrick fedha badala ya sisi kupata fedha. Ni jambo la fedheha mno, wanaojigamba kuwa ni wazalendo leo wametuuza.”

Ingekuwa nchi nyengine, Zitto ambaye kitaaluma ni mchumi anasema, “makubaliano haya ya Kimangungo kati ya Serikali ya Rais Magufuli na kampuni ya Barrick, ingetosha kuiondoa Serikali madarakani.”

Anasema, “Rais Magufuli na waziri Kabudi wameuza nchi yetu kwa kipande cha dhahabu. Wamelihujumu taifa.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!