NYOTA ya Camilius Wambura, ndani ya Jeshi la Polisi Tanzania, imeendelea kung’aa, baada ya Amri Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan, kumpandisha cheo kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) kuwa Kamishna wa Polisi (CP). Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).
Pia, Rais Samia amemteua Kamishna Wambura kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), akichukua nafasi ya Robert Boaz.
Ni ndani ya kipindi cha takribani wiki mbili, ambapo Wambura alikuwa Mkuu wa Operesheni Dodoma na sasa anakuwa DCI.
Mabadiliko hayo ndani ya Jeshi la Polisi, yametangazwa, leo Jumatatu, tarehe 31 Mei 2021 na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu.
Kabla ya uteuzi huo, Wambura alikuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, nafasi aliyohudumu kwa takribani wiki mbili kuanzia tarehe 17 Mei 2021, akichukua nafasi ya Lazaro Mambosasa.

Mabadiliko hayo, yalifanywa na Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro ambapo, Mambosasa alimpeleka kuwa Mkuu wa Operesheni Dodoma.
Taarifa hiyo ya Msigwa imesema, Rais Samia amempandisha cheo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Hamad Khamis Hamad kuwa Kamishna wa Polisi (CP).
Wambura, amewahi pia kuwa Kamanda wa Polisi Kinondoni mkoani Dar es Salaam na baadaye kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Pamoja na kumpandisha cheo, Rais Samia amemteua Hamad kuwa Mkuu wa Kamisheni ya Fedha na Lojistiki wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Kabla ya uteuzi huo, CP Hamad alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.
Leave a comment