May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shahidi asita kujibu maswali ya kina Mbowe, kesi yahairishwa

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, imeahirisha kwa muda kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, ili ijipange kutoa uamuzi wa pingamizi la Jamhuri, dhidi ya ombi la upande wa utetezi la mahakama hiyo kumuamuru Luteni Denis Urio, ajibu maswali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tukio hilo limetokea leo Alhamisi, tarehe 27 Januari 2022, mahakamani hapo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, wakati Luteni Urio akiulizwa maswali ya Dodoso na Wakili wa utetezi, Nashon Nkungu.

“Mme-cite (taja) sheria kadhaa ili niweze kutoa maamuzi stahiki, nahitaji muda kidogo nipitie. Naomba niahirishe kwa muda nipitie sheria ili nije kutoa maamuzi,” amesema Jaji Tiganga.

Upande wa utetezi ulimuuliza Luteni Urio, maswali yaliyomtaka aeleze baadhi ya taratibu za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo yenye mashtaka ya ugaidi ni, waliokuwa makomandoo wa JWTZ, Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Miongoni mwa maswali aliyokataa kujibu kwa sababu za kiusalama na siri ya kiapo chake ni, kutaja idadi ya vituo vya kijeshi vinavyofundisha mafunzo maalum ya ukomandoo.

Ambapo alikataa kujibu akidai kwa sababu za kiusalama, kwa kuwa kesi hiyo inafuatiliwa na watu wengi ndani na nje ya Tanzania.

Maswali mengine aliyokataa kujibu kwa sababu za kiusalama, ni lile alilotakiwa kueleza JWTZ inazalisha makomandoo wangapi.

Baada ya kukataa kujibu maswali hayo, Wakili Nkungu alimuomba Jaji Tiganga atoe amri kwa shahidi huyo ili ajibu maswali yake, akidai kitendo hicho ni kinyume cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho 2019, kifungu cha 264 sura ya 20.

Ombi hilo lilipingwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, aliyedai ombi la Wakili Nkungu halina mashiko kisheria, kwa kuwa maswali yake hayahusiani na kesi iliyopo mahakamani.

Pia, amedai kutokana na sababu zilizotolewa na Luteni Urio kukataa kujibu maswali hayo, mahakama haina mamlaka ya kumlazimisha shahidi ajibu maswali hayo.

“Jaji masuala ya kiushahidi kupokelewa kwa ushahidi mahakamani kuna sheria yake mahususi ambayo ni Sheria ya Ushahidi, sura ya 6 iliyofanyiwa marekebisho 2019 na sheria hiyo ina kifungu mahususi kinachoelekeza ni mazingira yapi shahidi anaweza akaiomba mahakama kujibu swali,” amedai Wakili Chavula na kuongeza:

“Kifungu cha 158 cha sheria hiyo, kimeeleza ni wakati gani na mazingira yepi mahakama inaweza kumlazimisha shahidi kujibu swali.”

Freeman Mbowe akiwasili mahakamani

Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, amedai ni kinyume cha Sheria ya Usalama wa Taifa Kifungu cha 4 (1), kinachomkataza mtu kutoa taarifa ambayo ni siri ya Jeshi.

“Ni kosa la jinai na haruhusiwi na kwa kuwa shahidi ameshaeleza kwa kiapo chake hatakiwi kutaja level ya mafunzo aliyoyapata, ni rai yetu Jaji wakili hatakiwi kumlazimisha shahidi kueleza. Kuna maswali mengine shahidi kaeleza ana kiapo cha kutoyajibu,” amedai Wakili Hilla.

Baada ya mawakili hao wa Jamhuri kutoa mapingamizi hayo, Wakili Nkungu aliiomba mahakama iyatupilie mbali akidai hayana mashiko, kwa kuwa maswali aliyoyauliza yanaruhusiwa kujibiwa na sheria ya ushahidi, pia yana uhusiano na kesi iliyokuwepo mahakamani.

“Nimeshangaa kupingwa maswali ya identity (utambulisho) ya shahidi, hakuna sheria imetolewa kinyume na hiyo information (taarifa) ya shahidi kutolewa, isipokuwua Sheria ya Ushahidi kifungu 155 (B) yenyewe ndiyo inaruhusu kwamba shahidi akiulizwa maswali shahidi yeye ni nani na posistion yake ni ipi,”amedai Wakili Nkungu.

“Jaji naona sheria inaruhusu, swali langu halihusiani na taarifa inayotakiwa isitolewe mahakamani. Hakuna sheria imetaja kukataza information hiyo kutolewa kutoka kwa shahidi, hivyo narudia ombi langu la kuomba shahidi kujibu swali langu nililotoa,”

Maswali ya Wakili Nkungu na Luteni Urio, yaliyoibua mvutano huo wa kisheria, yalikuwa kama ifuatavyo;

Nkungu: Moja ya vitu ambavyo umekuja kueleza mahakamani kwamba kikosi cha 9KJ inatrain wanajeshi wa mafunzo maalumu, yaani ukamondoo, tuambie Tanzania kuna vituo vingapi?

Shahidi: Siwezi kulijibu hilo swali, kwa sababu ya usalama

Nkungu: Kwa sababu ya usalama upi?

Shahidi: Naomba nirejee maneno yako, hii kesi inafuatalia ndani na nje ya nchi nikitaja itakuwa si sahihi.

Nkungu: Wakati unataja Kikosi cha Jeshi cha 92 KJ, hukujua kesi inafuatiliwa ndani na nje ya nchi?

Shahidi: Najua

Nkungu: Basi vitaje vingine viko vingapi jumla?

Shahidi: Kwa mujibu wa kiapo changu siwezi kuvitaja.

Nkungu: Wewe ulifuzu mafunzo yako ya mwisho ya ukomandoo lini?

Shahidi: Siwezi kuongelea

Nkungu: Mafunzo ya mwisho ulipata lini?

Shahidi: 2010

Nkungu: Ilikuwa level gani?

Shahidi: Bado siwezi kusema.

Nkungu: Jaji naomba umuarumu shahidi huyu ajieleze, hataki kujieleza yeye ni nani. Inaonekana ni mtiririko ambao amepanga kuzuia kumhoji kwa mtiririko huu.

error: Content is protected !!