May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askari JWTZ adai Mbowe alimpa Sh 699,000 amtafutie makomandoo

Spread the love

 

LUTENI Denis Urio, shahidi wa 12 wa Jamhuri, amedai Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katika nyakati tofauti alimpatia Sh. 699,000, kwa ajili ya kumtafutia waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ili wamsaidie katika harakati za chama chake kuchukua dola 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Luteni Urio ambaye ni Askari wa JWTZ, ametoa madai hayo leo Alhamisi, tarehe 27 Januari 2022, akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdllah Chavula, katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili mwanasiasa huyo na wenzake, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi yenye mashtaka ya ugaidi inayosikilizwa mbele ya Jaji Joachim Tiganga, ni Halfan Bwire Hassa, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya. Wote waliwahi kuwa makomandoo wa JWTZ.

Luteni Urio amedai, Mbowe alikuwa anamtumia pesa hizo kwa njia ya simu, Julai 2020.

Askari huyo wa JWTZ, amedai kuwa alianza kufahamiana na Mbowe tangu 2008, hadi 2020 alipomkatia mawasiliano baada ya kumpatia vijana hao aliokuwa anawataka.

Kwa kujibu wa Luteni Urio, makomandoo hao waliopelekwa kwa Mbowe kufanya kazi ya ulinzi, ni washtakiwa wenzake na mwingine ambaye anaendelea kutafutwa, Moses Lijenje.

Haya hapa mahojiano kati ya Wakili Chavula na Luteni Urio;

Chavula: Ulisema Mbowe ulifahamiana naye 2008 hadi 2020, ulikuwa unamaanisha nini?

Shahidi: Nilifahamiana naye mpaka 2020, nilikuwa na maana kwamba baada ya kupata vijana wa kumsaidia harakati za kuchukua dola, ndiyo alikata mawasiliano na mimi, ilikuwa tarehe 24 Julai 2020.

Chavula: Hebu tuambie ukaribu wenu wewe na yeye kiujumla yalikuwaje?

Shahidi: Ulikuwa mazuri japo alikata mawasiliano na mimi, sijui kwa nini alikata mawasiliano na mimi, lakini tulikuwa na mawasiliano mazuri.

Chavula: Iambie mahakama jumla ya kiasi gani cha fedha ulichopokea kutoka kwa Mbowe kuwapelekea wale watu?

Shahidi: Jumla 699,000

Katika kesi hiyo yenye mashtaka sita ya ugaidi, Mbowe anadaiwa kutoa Sh. 699,000 kwa ajili ya kufadhili vitendo vya ugaidi.

Mengine ni kupanga njama za kudhuru viongozi, kuanzisha maandamano yasiyo na kikomo, kulipua vituo vya mafuta na maeneo yenye mikusanyiko ya watu.

Kwa mujibu wa ushahidi wa Luteni Urio, Mbowe alipanga njama za kutekeleza vitendo hivyo kwa msaada wa makomandoo hao, ili kuchukua dola kwa gharama yoyote katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Mbowe na wenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai na Agosti 2020, katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Kilimanjaro.

Shahidi huyo anaendelea kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji Tiganga, ambapo mawakili wa utetezi wanamuuliza maswali ya dodoso.

error: Content is protected !!