WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Selemani Jafo amesema ushirikishwaji wa wadau katika ngazi zote na matumizi bora ya maji ya mvua zinazoendelea kunyesha ni mojawapo ya mikakati endelevu ya kuigeuzia Dodoma kuwa ya kijani. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea)
Jafo ametoa kauli hiyo jana tarehe 26 Januari 2022 alipokutana na wadau wa mazingira wa Jiji la Dodoma kutoka sekta binafsi na taasisi za Serikali.
Mkutano huo ulilenga kuweka mikakati ya pamoja katika kutekeleza kwa vitendo kampeni ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.
“Zoezi la kuigeuza Dodoma ya kijani linaendelea kwa kupanda miti maeneo mbalimbali ya jiji la Dodoma ambapo zaidi ya miti 40,000 imeshapandwa katika maeneo ya viwanja vya Chuo kikuu cha Dodoma, Mji wa Serikali Mtumba, Eneo la Medeli na maeneo ya kuzunguka Shule za Msingi na Sekondari zilizopo Dodoma” Dk. Jafo alisisitiza.
Pia ametoa wito kwa jamii kufuata taratibu na kuzingatia sheria na kuacha kujishughulisha na shughuli zisizoendelevu ikiwemo uchomaji wa moto hovyo katika maeneo mbalimbali, hususan maeneo ambayo miti inapandwa.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Edward Nyamanga ametoa wito kwa sekta binafsi na wafanyabiashara wa aina mbalimbali Jijini Dodoma kushiriki kwa dhati katika kuunga mkono serikali kwenye azma yake ya kuifanya Dodoma kuwa Jiji la mfano nchini katika masuala ya Hifadhi na Usafi wa mazingira.
Amesema lengo la kuanzishwa mpango wa kupanda miti wa kulifanya jiji la Dodoma kuwa la kijani ni kuhakikisha kuwa maeneo ya wazi, pembezoni mwa barabara, makazi pamoja na maeneo ya kuzunguka mashamba yanapandwa miti ili kuhifadhi mazingira na kupendezesha jiji la Dodoma.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe amesema zoezi la upandaji miti liwe endelevu na kutoa rai kwa Serikali kuepuka zoezi la upandaji miti wakati wa maadhimisho na sherehe za kitaifa pekee.
Leave a comment