May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Samia aota uchaguzi mkuu 2025

Spread the love

 

MWENYEKITI mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho, kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho (2020-2025), kwani ndio mbinu ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa 2025. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Samia ambaye pia ni Rais wa Tanzania, ametoa wito huo leo Ijumaa tarehe 30 Aprili 2021, saa kadhaa baada ya kupitishwa kwa asilimia 100 kuwa mwenyekiti wa CCM. Samia amechaguliwa na wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho, uliofanyika jijini Dodoma.

Mwanamama huyo amechaguliwa kurithi mikoba ya Hayati Dk. John Magufuli, aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, kwa ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam.

Samia amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM, kuendelea na majukumu ya kukiongoza chama hicho yaliyoachwa na Dk. Magufuli, ambaye alikabidhiwa uenyekiti wake 2017 nafasi aliyoihudumu hadi Machi 2022.

Hivyo, mwenyekiti huyo ataiongoza CCM kuanzia sasa (2021) hadi 2022 ambapo muhula wake utakoma. Ni kwa kuwa, miaka mitatu na miezi kadhaa imetumiwa na mtangulizi wake Hayati Magufuli.

“Sisi ndiyo tuliyopewa dhamana na wananchi, hivyo tunawajibu kuhakikisha serikali inatekeleza ahadi tulizozitoa, na katika hilo nawaomba WanaaCCM tukumbe kuwa, ushindi kwenye uchaguzi wa 2025 utaletwa kwa namna tutakavyotekeleza ilani tuliyoinadi kwa Watanzania,” amesema Samia.

Amesema, kila MwanaCCM ana wajibu wa kuisimamia serikali, ili itekeleze ahadi zake ilizotoa kwa wananchi.

“Naomba niwakumbushe kuwa mwezi Oktoba mwaka jana nchi yetu ilifanya uchaguzi mkuu, katika uchaguzi huo Watanzania walitupa dhamana ya kuliongoza Taifa, sasa jukumu letu kuhakikisha yale tuliyoahidi kupitia ilani yetu tunayatekeleza,” amesema Samia.

Mrithi huyo wa Dk. Magufuli amesisitiza “hivyo basi, kila mwanaCCM ana wajibu kuhakikisha anaisimamia Serikali ili tutekeleze ahadi tuliyotoa kwenye uchaguzi mkuu 2020, niwaombe ndugu zangu wana CCM  kuhakikisha ilani tuliyonadi inatekelezwa kwenye maeneo yetu.”

Aidha, Samia ameonya viongozi wa CCM kutowachonganisha viongozi wa Serikali na wananchi.

“Katika kutimiza wajibu huu, tunatakiwa kufahamu njia bora za mawasiliano ili tuwe kiungo baina ya wanachama wetu na vyombo vya serikali,” amesema Samia na kuongeza:

“…na hapa nitoe angalizo kwa viongozi wa CCM katika ngazi zetu mbalimbali, kuacha kuwa sehemu ya kutengeneza migogoro baina ya watendaji wa serikali na wananchi, bali tuwe daraja kusaidia wananchi wa maeneo yetu kupata huduma inayostahiki.”

error: Content is protected !!